Sare sio kigezo mtoto kutokwenda shule

WAZAZI na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuwapeleka watoto wao shule hata kama wahawajakamilisha utaratibu wa upatikanaji wa sare.

Akizungumza wilayani humo jana Januari 8, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda amewataka walezi hao kutekeleza agizo hilo la serikali kuanzia jana Januari 8, mwaka 2024.

Advertisement

‘’Sisi tumesema hata kama haujakamilisha yunifomu, yunifomu haisomi anayesoma ni mtoto, mlete wakati bado unaendelea kujipanga kununua yunifoma ila tujitahidi kuwakamilishia mahitaji yao wakati mtoto anaendelea kuja shuleni.’’amesema Munkunda

Aidha akiwa katika shule ya msingi Chawi iliyopo Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wilayani humo DC Munkunda amemuagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo kutomkataa mtoto yoyote ambaye mzazi wake hajakamilisha utaratibu huo.
‘’Wazazi, viongozi wenzangu tuwalete watoto shule, kwa idadi ambayo tumeipokea bado kwa kuwa watoto wanaendelea kuletwa lakini sisi tumesema hata kama haujakamilisha yunifomu, yunifomu haisomi anayesoma ni mtoto.’’amesema Munkunda.

Ofisa Elimu wa kata ya Chawi kwenye halmashauri hiyo, Zaina Hassan ameipongeza Serikali kwa kuwajengea shule mzuri kwa sababu awali kabla haijajengwa shule hiyo alikuwa akisimamia shule ambayo miundombinu yake ni chakavu.

‘’Kwa kutuletea fedha ya kujenga shue hii mpya nina uhakika walimu wangu, wanafunzi na jamii kwa ujumla wamefurahi sana kwa kupata huu mradi unaowezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri’’amesema Hassan.

Mwanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo, Hamisi Rashidi ‘’Tunamshukuru mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea majengo mapya katika shule yetu kwasababu mwanzo tulikuwa tunasomea kwenye majengo ambayo mvua ikinyesha tunakaa pembeni’’

Aidha, mwanafunzi huyo amesisitiza kuwa, kutokana na kuwepo kwa majengo mazuri shuleni hapo, ameahidi kufanya vizuri katika masomo yao na kuleta matokeo mazuri kwa shule hiyo.