Saruji Mbeya yapewa siku 30 kurekebisha mazingira ya kazi

SERIKALI imetoa siku 30 kwa uongozi wa kiwanda cha saruji cha Mbeya kiboreshe mazingira ya kazi kwa wafanyakazi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Patrobas Katambi alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda hicho na kubaini kuwa mazingira ya kazi si salama kwa wafanyakazi.

Katambi aliongozana na maofisa wa serikali wakiwemo kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), maofisa kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na maofisa wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA).

Alisema katika baadhi ya maeneo hasa ya uzalishaji vumbi linatimka na wafanyakazi hawana vifaa vya uhakika vya kujikinga hivyo wapo hatarini kupata magonjwa na ulemavu.

Katambi aliagiza viongozi wa kiwanda hicho watafute mitambo ya kisasa zaidi ambayo wakati wa uzalishaji haizalishi vumbi ili kupunguza madhara kwa wafanyakazi.

“Kuna sehemu nimekuta mmoja wa wafanyakazi amevaa barakoa ambayo inaonyesha ameitumia muda mrefu sana, imechoka na haiwezi tena kumsaidia, sasa hakikisheni mnarekebisha hali hiyo haraka,” alisema

Katambi alisema ilitakiwa akitoze faini kiwanda hicho lakini alisamehe kutokana na kushtukiza na hivyo akasema endapo hawatarekebisha watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kutozilipa kampuni wanayofanyanayo kazi kama hazitekelezi sheria za nchi na alishauri kwenye mikataba yao waweke kipengele kinachosisitiza utekelezaji wa sheria hizo.

Mwakilishi wa WCF Mkoa wa Mbeya, Ayoub Bendera alisema wamekuwa wakipata malalamiko ya magonjwa kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho.

“Tumekuwa tukipokea kesi nyingi sana za wafanyakazi kuugua wawapo kazini kwenye kiki kiwanda na tunalazimika kuwalipa fidia, kwa hiyo tunaomba waboreshe mazingira ya kazi,” alisema Bendera.

Kaimu Meneja wa OSHA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Uswege Faston alisema mpaka sasa hawajatoa cheti cha usalama na afya mahali pa kazi kwa kiwanda hicho kutokana na kutotimiza baadhi ya masharti.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Khaled Ghareib alisema wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya sheria za nchi lakini kwa sehemu kubwa wanakwamishwa na kampuni wanazofanya nazo kazi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button