KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imeitikia wito wa serikali na wadau wengine unaolenga kuzalisha maafisa ugani wengi zaidi watakaosaidia kuwaelimisha wakulima kuzalisha malighafi zenye ubora kwa ajili ya viwanda.
Kwa kupitia programu yao ya Kilimo Viwanda Scholarship inayolenga kutoa mafunzo ya kilimo kwa wanafunzi wanaopata changamoto ya kuendelea na masomo kutokana na sababu za kiuchumi, SBL imekwishatoa ufadhili wa masomo hayo ya kilimo kwa vijana zaidi ya 300.
Akitoa taarifa hiyo katika hafla ya kutoa vyeti kwa wanafunzi 14 wanaopata ufadhili katika Chuo cha Kilimo cha Mt. Maria Goletho kilichopo kata ya Ilula, wilayani Kilolo mkoani Iringa, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) Obina Anyalebenchi alisema:
“SBL tunafadhili programu hii ili kutoa fursa kwa wanafunzi wenye vipaji kutoka familia za kipato cha chini kufikia ndoto zao hasa katika sekta ya kilimo ambayo sisi wazalishaji wa vinywaji na bidhaa zingine tunategemea malighafi zenye ubora kutoka kwa wakulima.
Mbali na chuo hicho cha Mt. Maria Goleth, alisema kampuni yao inaendesha pia program hiyo kupitia vyuo vingine vya Kilimo na mifugo kikiweno cha Kaole Bagamoyo, Kilalacha Moshi na Igabulo Bukoba.
Alisema program hiyo inawawezesha vijana hao kutoka familia za kipato duni kulipiwa ada, mafunzo kwa vitendo na kutafutiwa fursa mbalimbali ikiwemo mitaji katika vikundi kwa kuunganishwa na taasisi mbalimbali za kifedha ili wapate mikopo ya kuanzisha mashamba yao.
Awali mratibu wa mafunzo kutoka SBL NeemaTemba alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 program hiyo imekwisha wanufaisha wakiwemo 14 wa chuo hicho cha Mt. Maria Goletho cha Ilula.
Temba ametoa wito kwa wadau wengine kuwekeza katika kuzalisha maafisa ugani watakosaidia kutoa ushauri kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo, matumizi ya mbolea, na kudhibiti magonjwa na wadudu.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Chuo cha Mt.
Maria Goleth, Isaya Kigava alisema programu hiyo ni mkombozi wa vijana wengi na katika kipindi cha miaka mitano vijana 66 wamenufaika kupitia chuo chao.
Alisema kati ya vijana waliomaliza chuoni hapo wamepata ajira serikalini, taasisi binafsi, wengine kujiajiri na kujiendeleza hadi ngazi ya Shahada katika vyuo mbalimbali vya kilimo.
Kwa upande wake, ofisa ugani kata ya Masunzi, Ibrahim Kisweswe, amethibitisha kuwa mpango huu umeleta mabadiliko makubwa na kuongeza ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo.
Aliwahimiza vijana kuamini katika ndoto zao na kueleza kuwa kilimo kina fursa kubwa ikiwa watakipenda na kuwekeza nguvu zao katika sekta hiyo.
Mnufaika wa Programu, Sharifa Maketa, akishirikisha hadithi yake amesema ndoto zake zilikatishwa na ujauzito akiwa kidato cha tano na hakuwa na uwezo wa kujilipia ada mara baada ya kujifungua kutokana na uchumi kuwa duni lakini kwa kupitia program hiyo ameweza kutimiza ndoto zake.
“Nimemaliza Stashahada ya Kilimo na kupata ajira na naiomba kampuni hii ya Serengeti Breweries kuendelea kuunga mkono vijana wenye uhitaji kama mimi ili wafikie malengo yao,” alisema.
Alisema programu hiyo inaashiria mwanga mpya katika sekta ya kilimo nchini Tanzania, ikiwapa vijana matumaini na fursa ya kukuza ujuzi wao na kuchangia ukuaji wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.
Comments are closed.