‘School Bus’ zote kuwa na Konda wanawake,ni baada ya mtoto wa miaka 6 kubakwa

Kufungwa camera

KUBAKWA kwa mtoto wa miaka sita wa darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Star Light Pre and Primary School iliyopo Tegeta Wazo mkoani Dar es Salaam, serikali imeagiza mabasi yote yanayobeba wanafunzi kuwa na kondakta wa kike na mabasi yote yafungwe Camera maalum.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt. Dorothy Gwajima na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe walipofika katika shule hiyo  ambayo dereva na kondakta wa gari la shule wanatuhumiwa kumbaka mtoto wa miaka sita.

Akizungumza leo Novemba 30, 2022 Gwajima amesema “Watuhumiwa kwa sasa wapo ndani na wameshapanda mahakamani, pongezi wote waliowajibika haraka kesi inaendelea.”Amesema Gwajima

Amesema hakuna namna inabidi magari yote yanayobeba wanafunzi badala ya kuwa wanaume wawili mmoja dereva na mwingine kondakta, lazima mmoja awe mwanamke.

“Na hapa hakuna cha gharama kuongezeka maana jinsia tu ndio inabadilika. Hii itawezesha ulinzi imara kwa mtoto wa kwanza kuchukuliwa na wa mwisho kurejeshwa.” Amesema na kuongeza

“Huko mbele kuna haja ya kufunga camera kwenye mabasi ya shule tunaangalia uwezekano. Lazima watejwa walindwe yaani mtoto ni mteja jamani inakuwaje analipia huduma alafu anafanyiwa vitendo vya kikatli?” amesema kwa kuhoji

Tamko hilo la serikali linakuja ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii inayosema ‘Dereva na anko wabaka mtoto wa miaka sita’

Katika taarifa hiyo inaeleza kuwa wanaume wawili watu wazima ambao ni dereva na Konda ambaye maarufu ‘anko’ wa shule hiyo ya Starlight Pre and Primary school wamekuwa wakimbaka mtoto huyo kwa muda mrefu bila kuwaambia wazazi wake kwa sababu wabakaji hao walikuwa wakimtisha kuwa akisema watamuua.

Taarifa hiyo inasema kuwa mzazi wa mtoto huyo alibaini mtoto wake kufanyiwa kitendo hicho cha kikatili baada ya kulalamika mfululizo kuumwa na tumbo ndipo alipoanza kumdadisi jinsi anavyoumwa huku akimfanyia uchunguzi wa mwili.

“Siamini kwa sababu sikuwahi kufikiria wale watu wazima tena wa shule tunayoiamini kuwafuata watoto wetu nyumbani kuwapeleka shule na kuwarudisha wanaweza kufanya kitendo cha kikatili hivyo. Mtoto alikuwa haishi kulalamika kuumwa tumbo, nimempeleka Kitengule Hospitali zaidi ya mara tano, tunapewa dawa lakini malalamiko ya kuumwa tumbo hayaishi.

“Majuzi akaanza kulia tena tumbo linamuuma, nikachanganyikiwa kabisa maana kila nikienda hospitali hawaoni tatizo, nikaamua kukaa naye chini kumbembeleza huku nikimuuliza tumbo linaumaje, akawa anasita kusema, hapo akili ikashtuka.

“Nikazidisha utulivu huku nikimbembeleza asilie bali aseme linaumaje akasema anaogopa kwa sababu watamuua, nikamuuliza akina nani, hakusema. Nikamwambia hakuna wa kumuua mimi nipo na baada ya kumbembeleza sana ndiyo akaanza kusema dereva na ‘anko’ wa gari lao la shule yaani ‘school bus’ huwa wanambaka, wanambaka kwa zamu.

“Alieleza kila kitu, alisema wanavyomshika mpaka wanavyomvua nguo na wao wanavyovua. Alisema wakati wanamrudishwa nyumbani kutoka shuleni watoto wote huwa wanapelekwa kwanza anabaki yeye peke yake kwenye gari, kisha gari linapelekwa eneo la ukimya, wanafunga vioo na mapazia ya kwenye vioo vya gari ndiyo wanamtendea huo unyama, wakimaliza ndiyo wanamrudisha nyumbani huku wakimtisha kuwa akisema watamuua,” alisema mzazi wa mtoto huyo na kuongeza.

“Usiku ule ule tulimpeleka hospitali akapata matibabu ya awali na wakatuambia ni kweli kaishaharibiwa kabisa. Tuliwasiliana na polisi usiku huo huo wakawahi nyumbani asubuhi asubuhi ile gari ya shule ilipofika tu yule dereva akatiwa nguvuni ila huyo mwenzake alikamatwa baadaye wakapelekwa kituo cha polisi cha Madale, kesi namba iliyofunguliwa ni MDL/RB/3889/2022, KUBAKA.

Hivi sasa tunaendelea na matibabu ya mtoto katika Hospitali ya Mwananyamala.

 

 

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button