SDF wajivunia kazi za waliopata mafunzo

OFISA Miradi na Mratibu Msaidizi wa Mfuko wa kuendeleza Ujuzi Tanzania (SDF), Lusungu Kaduma amesema wanajivunia kazi zinazofanywa na wanufaika waliopata mafunzo, kwani wengi wameweza kunufaika kutokana na kuzalisha bidhaa zinazofanya vizuri kwenye soko.

Akizungumza kwenye maonesho ya Wiki ya Ubunifu kitaifa yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Kaduma alisema kuwa suala la kuwapatia vijana ujuzi ni la msingi, ili waweze kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.

Alisema kupitia mafunzo yanayotelewa wijana wengi wameweza kufikiwa na kupwatiwa mafunzo ya kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza wigo wa vijana kujiajiri na kuajiri wengine.

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha vijana wanakuwa na shughuli ambazo zina uwezo wa kuwaingizia vipato na hivyo kutoa mchango wao katika taifa.

Mmoja wa wanufaika wa Mfuko wa SDF, Gishom Munyi kutoka mkoani Iringa alisema kuwa amekuwa mzalishaji wa vyakula ikiwemo viungo (spices) na kwamba bidhaa hizo zinafanya vizuri sokoni kutokana na kuwa na ubora mzuri.

“Niliamua kuwa msindikaji wa viungo vya aina mbalimbali, ikiwemo tangawizi vitunguu saumu, pilau masala, iliki na sasa natengeneza biskuti zenye ladha ya tangawizi, ambazo zinapendwa na watu wengi,” alisema

Alisema kuwa tangawizi imekuwa na faida nyingi mwilini ikiwemo kuboresha afya ya uzazi pia inasaidia kutibu kifua, kikohozi,.

Wageni waliotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), wakionja mvinyo uliotengenezwa na wanufaika wa SDF Lisa Mkuyu na Witnes Jacob katika maonesho ya Wiki ya Ubunifu yanayoendelea kwenye viwanja vya Jamhuri, Dodoma. (Picha na Sifa Lubasi).

Ofisa Habari wa Mfuko huo, Eliafile Solla alisema Mfuko wa  SDF ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta Tija katika Ajira (ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi nchini (NSDS).

Mfuko wa SDF ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), unapata ufadhili kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.

Solla alisema, SDF unatoa ufadhili kwa taasisi zinazolenga kutoa mafunzo ya Kuendeleza ujuzi ikiwemo SIDO, VETA, vyuo vya maendeleo ya jamii na za watu binafsi katika sekta sita za kipaumbele ambazo zinaratibiwa na ESPJ.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button