Sekondari Nyabange kuitwa Sagini

PENDEKEZO la Shule ya Sekondari Nyabange  kuitwa majina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini limepokewa vizuri na wanakijiji cha Nyabange, mkoani Mara.

Shule hiyo inajengwa Kata ya Nyankanga, ambayo inatakiwa kuanza usaili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza, Januari mwakani.

Pendekezo hilo lilielezewa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Husna Juma, akifungua Mkutano Mkuu wa Kijiji hicho,  akisema ofisi yake ililipokea kutoka kwa Diwani wa Kata hiyo, Jackob Shasha.

Naye Shasha alisema Sagini ni miongoni mwa wadau walioombwa kusaidia ujenzi wa boma lenye vyumba vinne, lililoanzishwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2016, akakubali.

“Ametutaka tujenge mpaka hatua ya kupauliwa, yeye atapaua na kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha kutumika na mimi kwa niaba yenu nikamuahidi shule iitwe Sagini,” alisema Shasha.

Pendekezo hilo lilipokewa vizuri na wanakijiji waliohudhuria mkutano huo, huku mikakati ya kuendeleza ujenzi huo, ikiwekwa na kuanza kutekelezwa.

Kwa upande mwingine, serikali imepeleka Sh milioni 40 za kuanzisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na kimoja cha ofisi, ili Januari mwakani, wanafunzi wa Kidato cha kwanza waanze wasailiwe.

Ili kupata vyumba vyenye ubora na vya kisasa, wanakijiji hao waliafikiana  kila kaya ichangie Sh 4,000 za kununulia kokoto, mchanga na mawe vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.

Naye Ofisa Elimu wa Kata hiyo, Mwita Ghati, alisema kila kidato kinahitaji kuwa na madarasa matatu, hivyo wanakijiji waliafikiana kuwa ujenzi wa vyumba vitatu uliyoanzishwa na serikali, utekelezwe sambamba na mikakati ya kukamilisha boma lenye vyumba vinne, mpaka hatua ya kupauliwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button