MBUNGE wa Dodoma mjini Anthony Mavunde amekabidhi vitabu 1667 kwa shule ya Sekondari ya Mtemi Chiloloma.
Vitabu hivyo vimetolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vitabu hivyo Mavunde amesema shule hiyo ni moja kati ya shule zilizojengwa kwa kila kata nchini, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Watoto wa hapa walikuwa wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 19 kufuata shule kata ya Hombolo Bwawani lakini sasa wanasomea hapa hapa,haya ni maendeleo makubwa.”Amesema Mavunde na kuongeza
“Nimesikia changamoto zenu za nguzo za umeme kufika hapa eneo la shule hili nitalishughulikia na tutawasha umeme. “
Aidha amehaidi kuwapatia vifaa vya michezo ambavyo ni magoli ya chuma,jezi na mipira na pia amehaidi kuchangia sh milioni 2.4 kwa ajili ya malipo ya walimu wanaojitolea.
Awali Mkuu wa shule hiyo Livinus Tanganyika amesema shule hiyo ambayo imeanza Oktoba,mwaka 2022 imejipanga kuhakikisha inatoa elimu bora ili kuwaandaa wanafunzi kutoa mchango wao kwa ustawi wa Taifa Tanzania.
Naye Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Hombolo Janeth kutonha ameishukuru serikali kwa ujenzi wa shuke hiyo pamoja na Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kwenye shughuli za maendeleo.