‘Sekta binafsi kichocheo kuimarisha utalii’

MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango, amesema serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi kama kichocheo cha kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini.

Kutokana na hali hiyo amesema, serikali  imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuleta mageuzi hususani katika sheria na maboresho ya sera ya bajeti, ili kusaidia ukuaji wa sekta hiyo.

Dk Mpango amesema hayo wakati akifungua onesho la sita la Swahili International Tourism Expo jijini Dar es Salaam.

Alitaja  hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali, ikiwemo kuboresha miundombinu ya huduma za utalii ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, kujenga na kukarabati barabara, viwanja vya ndege, kambi za watalii na kuongeza kasi ya Shirika la Ndege nchini ili kurahisisha safari.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amesema wizara hiyo imeweka malengo ya kuongeza watalii wasiopungua milioni 5, pamoja na kuongeza pato la taifa la dola bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

Amesema wizara imeendelea na jitihada kutangaza vivutio hususani katika ukanda wa kusini mwa Tanzania na kuwakaribisha wawekezaji na wadau wa utalii kuwekeza katika maeneo hayo.

Naye Waziri wa Utalii na Mambokale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Simai Mohammed Said, amesema ipo haja ya kuongeza jitihada na kuwekeza katika utalii wa urithi, ikiwemo kufanya tafiti na kuhifadhi maeneo ya urithi yatakayopatikana kupitia tafiti hizo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button