Sekta ya maji yaimarika miaka 2 ya Samia

WIZARA ya Maji imelieleza Bunge kuwa katika miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita kumekuwa na mafanikio katika sekta ya maji ikiwamo kukamilika miradi 1,373 ya usambazaji maji.

Waziri wa wizara hiyo, Jumaa Aweso amesema katika kipindi hicho hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama imeimarika kwa wananchi wa vijijini kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 77 Desemba, 2022.

Aweso alisema bungeni jijini Dodoma kuwa kwa upande wa maeneo ya mijini, hali hiyo imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 84 mwaka 2020 hadi wastani wa asilimia 88 Desemba mwaka jana.

Advertisement

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jana bungeni, Aweso alitaja miongoni mwa mafanikio katika miaka miwili iliyopita ni ukamilishaji wa miradi na kuchangia utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio katika vijiji 2,649 hivyo kufikisha vijiji 9,737 vyenye huduma ya maji nchini.

Alitaja mafanikio mengine ni kukamilika kwa miradi 80 ya usambazaji maji miji na kuanza kutoa huduma kwa wananchi 4,305,801 na kukwamuliwa kwa miradi 157 na kuanza kutoa huduma kati ya miradi 177 ya vijijini iliyokuwa na changamoto ya kutokukamilika kwa muda mrefu.

Aweso alitaja mafanikio mengine ni kukamilika utekelezaji wa miradi 218 kupitia fedha za Covid-19 inayohudumia wananchi milioni 2.09. Aliwaeleza wabunge kuwa miradi 44 imetekelezwa mijini na 174 vijijini.

Pia serikali imefanikiwa kuongeza maabara za ubora wa maji nchini zenye hadhi ya ithibati kutoka maabara moja ya Mwanza iliyokuwapo mwaka 2021 hadi kufikia maabara saba zilizopo Singida, Shinyanga, Kigoma, Bukoba, Musoma na Dar es Salaam.

Aweso alisema pia wameanza utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28 yenye thamani ya Sh trilioni 1.48 baada ya kusainiwa kwa mikataba ya ujenzi Juni mwaka jana.

Pia alisema wizara hiyo imeanza ujenzi wa Bwawa la Kidunda linalogharimu Sh bilioni 329.46 ili kuhakikisha maji yanapatikana katika kipindi chote cha mwaka katika Mto Ruvu ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.

“Pia tumeweza kukamilisha ujenzi wa mabwawa 10 ya ukubwa wa kati ya kuvuna maji ya mvua katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji hususani kipindi cha ukame,” alisema Aweso.

Alitaja mafanikio mengine ni kununuliwa na kuanza kutumika kwa seti 25 za mitambo ya kuchimba visima na seti tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa na wizara kukamilisha na kuanza kutoa huduma kwa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka miji ya Tinde na Shelui wenye uwezo wa kunufaisha wananchi 86,980.

Aweso alisema pia mafanikio mengine ni kukamilika mradi wa ujenzi wa choteo la maji kwa ajili ya mji wa Kigoma na kuwezesha wananchi 215,000 kupata huduma ya uhakika ya maji safi na salama.

Alisema pia wamekamilisha na kuanza kutoa huduma kwa mradi wa maji wa Kyaka-Bunazi, Wilaya ya Missenyi-Kagera ambao umewezesha wananchi 75,000 kupata huduma ya maji safi na salama.

“Pia kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa mradi wa kusambaza majisafi katika Mji wa Orkesumet wilayani Simanjiro unaonufaisha wananchi wapatao 52,000 pamoja na mifugo,” alisema Aweso.