‘Sekta ya uvuvi ina umuhimu mkubwa’

WAVUVI wapatao 197,763 wamepata ajira za moja kwa moja katika uvuvi hali inayoonesha kuwa sekta hiyo imekuwa na mafanikio makubwa hapa nchini.

Hayo yameelezwa na ofisa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dk Simon Kangwe katika Kongamano la Nane la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Dk Kangwe amesema takwimu hizo ni hadi kufikia Aprili mwaka huu na kwamba mafanikio hayo yametokana na uwepo wa TAFIRI.

Amesema wavuvi hao 197,763 wametumia vyombo vya kuvulia 58,448 vilivyowawezesha kuvuna zaidi ya tani 426.

Hilo limebainika wakati Dk Kangwe alipokuwa akichangia mada kuhusu mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya uchumi na kijamii nchini Tanzania katika sekta ya uvuvi.

Amesema kupitia sekta hiyo ya uvuvi zaidi ya Watanzania milioni 4.5 wameendelea kupata mahitaji yao ya kila siku kutokana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kuunda na kutengeneza boti, kushona nyavu, biashara ya samaki na mazao ya uvuvi ikiwemo baba na mama lishe.

“Pia sekta ya uvuvi huchangia katika usalama wa chakula nchini, ambapo samaki huchangia takribani asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama,” amesema.

Kwa maelezo ya Dk Kangwe katika mwaka 2021/2022, sekta hiyo ilichangia asilimia 1.8 katika Pato la Taifa na ilikua kwa asilimia 2.5.

“Shughuli za uvuvi zinafanywa zaidi na wavuvi wadogo wadogo kwenye maji ya asili ambapo huchangia takriban asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini,” amesema.

Amesema baada ya kuona hali ya uzaliaji wa kamba ipo chini ya wastani wa kilo 40 kwa saa, serikali ilifunga uvuvi huo kuruhusu kamba kuzaliana ikiwa ni pamoja na kuruhusu mazingira yaliyoharibiwa kujijenga.

Amesema hilo lilibainika baada ya kufanya utafiti na kubaini hali ya samaki hao aina ya kamba ipo chini utafiti ambao ulifanywa katika kanda kuu tatu za uvuvi huo katika eneo la Bagamoyo, ukanda wa delta ya Rufiji na Kilwa.

Amesema pia waliweza kufunga uvuvi wa pweza kwa miezi mitatu kwenye maeneo ya miamba, ili kuwawezesha kuzaliana na kukua, mafanikio ni kwamba wameweza kupatikana kwa wingi pweza wenye wastani wa zaidi ya kilo moja.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button