Sensa imerahisisha – Mavunde
NAIBU Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amepongeza zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka 2022 kwa kutoa takwimu za idadi ya wakulima katika maeneo mbalimbali kuanzia ngazi ya kitongoji na hivyo kuirahisishia kazi serikali katika kuwafikishia wakulima hao huduma za msingi.
Mavunde, ameyasema hayo katika viwanja vya stendi ya zamani Manispaa ya Singida akimuwakilisha Waziri wa Fedha Mipango Dk.Mwigulu Nchemba wakati wa maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika yaliyobeba kauli mbiu ya matumizi sahihi ya takwimu za kilimo ili kuboresha sera za uhimilivu wa kilimo, lishe na usalama wa chakula Afrika.
“Takwimu hizi juu ya idadi ya wakulima,umri, jinsi na mazao wanayozalisha inatupa nafasi serikali kusogeza huduma za msingi za kilimo kwa wakulima kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika.”Amesema
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo juu ya usajili wa wakulima wote nchini kwa lengo la kuhakikisha tunapata takwimu sahihi za wakulima na sisi wizara ya kilimo tumeendelea na zoezi hilo la usajili wa wakulima kwa lengo la kuwasajili wakulima zaidi ya milioni 8 kwa mwaka huu wa fedha.
“Hivyo Wizara ya kilimo itakaa pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ajili ya kutumia taarifa za pamoja za awali juu ya idadi ya wakulima na kuongeza kipengele muhimu cha kuonesha eneo shamba lilipo na ukubwa wake kwa kutumia vipimo mahsusi”Amesema
Akitoa maelezo ya awali, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema zoezi la sensa ya watu na makazi 2022 liliweka bayana kipengele cha kutambua shughuli za uzalishaji mali zinazozofanywa na wananchi ili serikali iweze kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kukuza sekta za uzalishaji mali za kilimo na ufugaji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameshukuru kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kufanyia maadhimisho hayo mkoani Singida,na kuahidi kwamba takwimu za shughuli za uzalishaji mali mkoani Singida watazitumia vizuri ili kuleta matokeo chanya kwenye kilimo hasa cha alizeti ambapo mwaka huu wa fedha wametenga takribani ekari 650,000 kwa ajili ya kilimo cha Alizeti.