Sensa kukamilika kwa ufanisi

Sensa kukamilika kwa ufanisi

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alisema mkoa huo hadi juzi kazi ya kuhesabu watu, sensa ilifikia asilimia 97.4 na walitarajia kuimaliza jana kwa ufanisi.

Chalamila alisema makadirio yaliyokuwa yamefanywa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ni kufikia kaya 644,655 za Mkoa wa Kagera na hadi Jumatatu saa 2 asubuhi kaya 631,858 zilikuwa zimefikiwa.

Alisema Jumanne mkoa huo unatarajia kuanza sensa ya makazi na itafanywa kwa siku tatu.

Advertisement

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema jana aliwataka makarani waliomaliza kuhesabu watu katika maeneo yao wahamie kwenye kaya za watu ambao bado hawajahesabiwa.

Mjema alisema hayo wakati akiwa kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo yaliyopo Mwime Kata ya Zongomela katika Manispaa ya Kahama.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas alisema jana ofisini kwake kuwa, sensa kimkoa ilikuwa imefikia asilimia 91 kwenye halmashauri zote tisa.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mtwara, Tamali William alisema sensa hii watu wengi walikuwa na utayari wa kuhesabiwa na leo itaanza sensa ya makazi.