Sensa muhimu katika katika kukuza uchumi

Sensa muhimu katika katika kukuza uchumi

HATUA ya serikali kuimarisha afya ya mama na mtoto na kupunguza idadi ya vifo vya uzazi, kuongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuongeza idadi ya Watanzania katika sensa ya mwaka huu ya watu na makazi.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) katika ukurasa wa 25, wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 62 mwaka 2015/16 hadi miaka 66 mwaka 2019/20.

Mchambuzi wa Masuala ya Diplomasia na Siasa wa Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, Abbas Mwalimu, anasema kuwa kupitia sensa ya mwaka huu, idadi ya Watanzania inaweza ikaongezeka zaidi kwa sababu mwaka 2012 idadi ya watu ilikuwa zaidi ya milioni 40.

Advertisement

Mwalimu anabainisha kuwa uamuzi wa serikali wa kuitangaza Agosti 23 mwaka huu kuwa siku ya mapumziko ilikuwa muhimu kuchochea na kuongeza hamasa ya wananchi kushiriki kuhesabiwa.

“Naamini mwaka huu idadi ya watu inaweza kufika hata milioni 70, sina shaka na hilo kwa sababu hata kiwango cha kuishi kimeongezeka, serikali imeimarisha afya ya mama na mtoto na kupunguza idadi ya vifo vya mama na watoto, imeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, hayo yote yanafanya afya ya Mtanzania kuimarika,” anasema Mwalimu.

Anasema ushiriki wa wananchi ni muhimu kwa kuwa nchi haiwezi kupiga hatua ya kimaendeleo pasipo kujua idadi ya watu kwa sababu mipango ya serikali inazingatia idadi ya watu. Mtakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Pastory Ulimali, wakati wa mkutano wa viongozi wa dini Juni mwaka huu jijini Dar es Salaam, alisema kuwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, sensa ya kwanza Tanzania ilifanyika mwaka 1967.

Ulimali alisema kuwa katika sensa yamwaka 1967, idadi ya watu ilikuwa milioni 12.3 na katika sensa zilizofuata ya mwaka 1978 idadi ya watu ilikuwa milioni 17.5, mwaka 1988 ilikuwa watu milioni 23.1, mwaka 2002 milioni 34.4 na mwaka 2012 ilikuwa milioni 44.9.

Ongezeko hili linatoa picha kwamba, sensa ya mwaka huu idadi ya Watanzania itakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na sensa zilizotangulia, hivyo kutoa ujumbe kwa serikali kujizatiti katika mipango yake ya maendeleo katika kuwahudumia watu wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti (REPOA), Dk Donald Mmari, anasema anatarajia sensa hii kutoa hali halisi ya idadi ya watu na kubainisha idadi na umri wa watoto, vijana, wanawake, wazee, watu wanaoishi vijijini na wanaoishi mijini.

“Taarifa hizi ni za msingi hata kwetu sisi tunaofanya utafiti kuona tujielekeze wapi kwenye kuangalia uhusiano kati ya rasilimali na idadi ya watu, shule, vituo vya afya na mengineyo,” anasema Dk Mmari.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Amina Msengwa, anabainisha kuwa sensa ni jambo muhimu la kitaifa katika kukuza uchumi.

Kwa umuhimu huu, Dk Msengwa anasema ni vyema Watanzania kuandaa na kutoa taarifa zao kwa usahihi ili ziwe na tija kwa mustakabali wa taifa. Baada ya kuhesabiwa pamoja na familia yake katika Kijiji cha Zogoali katika Kata ya Chanika,Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, amesema ushiriki wa wananchi katika sensa unaisaidia serikali kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo kwa watu wake.

“Ili tuweze kupanga vizuri rasilimali zetu, sensa inatuwezesha kujua kuna wananchi wangapi, kwa hiyo niwasihi Watanzania kutoa ushirikiano, tuwape taarifa zote muhimu vijana wanaouliza, huu ni wajibu wa msingi kwa taifa,” anasisitiza Dk Mpango.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, anasema kwa kuwa moja ya vipaumbele vya serikali yake ni kujenga uchumi wa buluu, sensa hii itasaidia kupanga mipango ya kuwasaidia wananchi wanaojihusisha na uchumi wa buluu.

Kwa kuwa serikali inawajibu kwa watu wake, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, anasema shabaha ya sensa ni kujua idadi ya watu wakiwemo watu wazima, vijana na watoto ili kuirahisishia serikali kupanga mipango ya kuwahudumia kwa kuwa kila kundi lina mahitaji yake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anasema takwimu zitakazopatikana si tu kwamba zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya nchi, bali pia zitalisaidia taifa kushiriki pamoja na mipango ya dunia kwa kuwa Tanzania ina marafiki wanaoiunga mkono katika mipango yake ya maendeleo.

Majaliwa anasema sensa ya mwaka huu ni ya aina yake kwa kuwa inahusisha uratibu wa mfumo wa anuani za makazi, inafanyika kidijiti kwa kutumia vishikwambi badala ya karatasi lakini pia hamasa ya Watanzania kushiriki kuhesabiwa nayo imekuwa kubwa.

“Naamini nitakapotoa taarifa ya mwisho ya tathmini ya mafanikio, tutakuwa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” anasema Majaliwa.