Sensa Tabora wavuka asilimia 100

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk Batilda Burian, amesema licha ya changamoto za mtandao, sehemu kubwa ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi, umefikia zaidi ya asilimia 100.

Amezungumza hayo katika kikao kazi cha Wadau wa Mitandao wa Kanda ya Kati, kilichoitishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kinachoendelea ndani ya ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

“Ukiondoa Wilaya ya Kaliua ambayo mpaka sasa (leo asubuhi) imefikisha asilimia 89 nayo ikifika jioni itakuwa imezidi asilimia 100, wilaya nyingine zote zimevuka asilimia zaidi ya 100,” amesema.

Advertisement

Balozi Burian amesema lakini kutokana na changamoto ya mtandao katika maeneo mengi ya Mkoa huo, takwimu hizo zinatofautiana na za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Amesema wakati mkoani takwimu zipo juu, NBS zinaonekana kuwa ndogo sana, hali aliyoielezea kuwa inawezekana kusababishwa na baadhi ya makarani kushindwa kupeleka kwa wakati taarifa kwa kutumia vishikwambi wanavyotumia, kwa sababu ya changamoto za mtandao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, pamoja na mengine ameahidi kuchukua hatua stahiki kuhusu kuboresha mawasiliano mkoani humo, akisema ufuatiliaji wao umebaini Tabora inaongoza kwa kuwa na wamiliki wengi wa laini za simu.

/* */