Sensa ya watu kuendelea siku saba

SENSA ya makazi inaanza leo na itafanywa kwa siku tatu, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda amesema.

Makinda alisema haya Jumatatu Dar es Salaam kazi hiyo itakwisha Septemba Mosi na kitakachofanyika ni kukusanya taarifa za majengo ya makazi na yasiyo ya makazi nchi nzima ili kuboresha sera na kupanga mipango ya kimkakati ya kuboresha sekta ya nyumba.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani waliowahesabu katika maeneo yenu kwa kutoa taarifa sahihi za majengo. Makarani waliofanya Sensa ya Watu na Makazi ndio hao hao watapita kwenye majengo yote yaliyopo kwenye maeneo ya kuhesabia watu ili kukusanya taarifa za majengo,” alisema.

Makinda aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hadi jana kazi ya kuhesabu watu ilikuwa ikiendelea vizuri na kwamba asilimia 93.45 ya kaya zilikuwa zimehesabiwa.

Alisema taarifa zilionesha asilimia 6.55 ya kaya zilikuwa hazijahesabiwa na akaomba wananchi ambao hawajahesabiwa watoe ushirikiano kwa makarani wa sensa.

Makinda alisema kama kuna watu hawakuhesabiwa hadi jana waende kwenye ofisi za serikali za mitaa na kuonana na mwenyekiti au mtendaji wa mtaa na kuwaachia namba ya simu ili karani amfuate alipo na kumhesabu.

Alisema kwa maeneo ya vijijini mwananchi ambaye hajahesabiwa aende kwenye ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji anachoishi aache namba ya mawasiliano ili makarani wamfuate alipo.

“Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa namba maalumu za mawasiliano kwa ajili ya wananchi ambao hawajahesabiwa kupiga simu moja kwa moja makao makuu Dodoma ili utaratibu wa kupeleka karani eneo husika ufanyike kwa wakati. Namba hizo ni:- 0753665491, 0764443873, 0626141515, 0784665404 na 0656279424,” alisema Makinda.

Alisema namba hizo zitaanza kutumika leo hadi Septemba 5 mwaka huu ili kumwezesha mwananchi kupata haki yake ya msingi ya kuhesabiwa.

Namba hizo zitawekwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa anwani www.nbs.go.tz na zitasambazwa pia katika mitandao ya kijamii ili ziwafikie wananchi wengi iwezekanavyo,” alisema Makinda.

Alihimiza kamati za sensa ngazi ya mkoa, wilaya, kata, kijiji na mtaa zitoe namba za mawasiliano ili wananchi wapige simu kueleza waliko ili utaratibu ufanyike wa kupeleka karani wa sensa akawahesabu.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button