JESHI la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, limepongezwa kwa kueezesha watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mratibu wa Sensa wa Manispaa hiyo, Joseph Ochora kwa askari wa dawati hilo, WP Herieth Samso baada ya kuwahesabu watoto 21, usiku wa kuamkia Leo.
“Tumeanzia hapa kwenye Mtaa wa Mwigobero A, Kata ya Mwigobero, ambapo kwa ushirikiano na Dawati la Jinsia la Polisi tumehesabu watoto 21, tunaelekea kwingine,” alisema Ochora.
Naye WP Herieth alisema amekuwa na desturi ya kukusanya watoto hao na kuzungumza nao masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao, hali ambayo imesababisha kuwa karibu nao, wakimchukulia kama mama yao.
Alisema mazingira hayo yalimuwezesha kuwashawishi na kuwaunganisha na familia zao, akitoa mfano kwamba mwaka 2019 alikuwa na watoto 60 wa mitaani, lakini sasa wamebakia 20 baada ya wengine kukubali kurejea kwenye familia zao.
Alisema suala la Sensa ya Watu na Makazi lilipotangazwa, alianza kuwajengea uelewa na kuwashawishi, ili wawe tayari kuhesabiwa, jambo ambalo lilihitimishwa usiku kwa watoto hao kushiriki kikamilifu.
Alitaja kiini cha kuwapo watoto wa mitaani kuwa ni ukatili wanaofanyiwa ndani ya familia zao na alitoa wito kwa jamii kuwapenda watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu, ili wawawezeshe kuwa katika misingi sahihi.
Naye mmoja wa watoto hao, Idd Khamis aliishukuru serikali kwa kuwakumbuka katika Sensa ya Watu na Makazi, kwani wamebaini kuwa hata wao wanakubalika kwa serikali na kuwekwa katika mipango ya maendeleo ya taifa.
“Tunafahamu kuwa tumehesabiwa, ili serikali ijue tupo wangapi, ikitokea ugonjwa unaohitaji dawa na sisi tunahusishwa kwa sababu idadi yetu tunaoishi kwenye mazingira magumu inajulikana,” alisema Khamis maarufu Mwanaharakati.