Sera ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar yakamilika

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesema rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Vijana imekamilika, na lengo lake kubwa ni kuliwezesha kundi hilo kujitegemea na kuendeleza miradi itakayoongeza ajira.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita wakati alielezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 pamoja na mpango kazi wa bajeti ya nusu mwaka katika Makao Makuu ya CCM Kisiwandui Unguja.

Tabia alisema rasimu ya maendeleo ya vijana itahusisha mipango mbalimbali ikiwamo uimarishaji wa Baraza la Vijana na majukumu yake ya kuliendeleza kundi hilo alisema jumla ya vijana 2,132 wanatarajiwa kufikiwa kwa kuibua miradi mbalimbali ya uchumi na uzalishaji mali ambayo itazalisha ajira.

Alisema tayari ipo miradi mbalimbali ambayo vijana wanatakiwa kuibua kwa ajili ya utekelezaji wake na hivyo kujiajiri katika sekta binafsi. “Katika maboresho ya sera ya vijana tumejipanga zaidi kuona mabaraza ya vijana yanafanya kazi zake vizuri katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Unguja na Pemba na kuibua miradi ambayo watajiajiri katika sekta binafsi,” alisema.

Katibu wa Baraza la Vijana Zanzibar, Salum Issa Makame alisema kuwapo kwa marekebisho ya sera ya vijana ni muhimu yatakayosaidia kuwapo kwa ushirikishaji mkubwa wa Baraza la Vijana kwa wananchi wengi wa makundi tofauti. Alisema tatizo ni mwamko wa vijana kwani ni vijana wachache ndio wanajiunga katika mabaraza ya vijana na hivyo kundi hilo kushindwa kushirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ambayo itawapatia ajira.

Habari Zifananazo

Back to top button