WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imelieleza Bunge kuwa tathmini imeonesha misingi ya sera ya mambo ya nje bado inakidhi matakwa ya sasa na ya baadaye.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Stergomena Tax alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Wizara hiyo iliomba Bunge liidhinishe zaidi ya Sh bilioni 247.97 na kati ya hizo, Sh bilioni 17.88 zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Dk Tax alisema wizara hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 na ili kuendana na mabadiliko katika uhusiano wa kimataifa na mambo ya nje, wizara ilifanya marejeo ya sera hiyo.
Alisema wizara imefanya tathmini kupima iwapo misingi na malengo ya sera ya mambo ya nje vinakidhi mahitaji ya sasa baada ya zaidi ya miaka 20.
“Napenda kulitaarifu bunge lako tukufu kuwa, tathmini hiyo imebainisha kuwa misingi ya sera iliyopo bado inakidhi matakwa ya sasa na ya baadaye,” alisema Dk Tax na akasema tathmini inaonesha yapo maeneo mapya yanayohitaji kujumuishwa katika sera hiyo.
Alitaja maeneo hayo ni kulinda uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe; kuheshimu mipaka ya nchi na uhuru wa kisiasa na kulinda uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia.
Dk Tax alitaja maeneo mengine ni kukuza ujirani mwema, kuendeleza Umoja wa Afrika (AU), kukuza ushirikiano wa kiuchumi na wabia wa maendeleo na kuunga mkono utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote.
Dk Tax alisema maeneo mengine ni kuimarisha ushirikiano wa nchi zinazoendelea na kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada za kuimarisha maendeleo ya uchumi wa kimataifa, amani na usalama.