DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema inafanya mapitio ya sheria na sera zilizopitwa na wakati katika tasnia ya habari na itakwenda kufanyia kazi changamoto za wanahabari wanawake, ikiwemo suala la ukatili na rushwa ya ngono.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew katika Maadhimisho ya Miaka 36 ya Chama Cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA)
Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameilekeza wizara hiyo kufanya mapitio ya sera kwa lengo la kuhakikisha tasnia ya habari inafanya vizuri zaidi.
“Chama hiki (TAMWA) kina mchango mkubwa kwa taifa, ikiwemo kupinga ukatili, kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na usawa wa kijinsia”amesema
Amesema Rais Samia ameielekeza wizara hiyo kufanyia kazi sera na sheria zilizopitwa na wakati, na kueleza kuwa katika sheria ambazo zitaenda kutungwa mawazo na maoni (TAMWA) yamechukiliwa na serikali itayafanyia kazi.
“Tasnia ya habari imekuwa na changamoto nyingi na Wizara inaendelea kushughulikia kama mabadiliko ya sheria ili kuweza kukidhi upatikanaji wa habari,”amesema na kuongeza
” Serikali inaendelea kuhakikisha kuna uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari, ndio maana tangu Rais Samia aingie madarakani hakuna chombo wala mwandishi wa habari aliyefungiwa”amesema
Aidha, amesema katika kuhakikisha wanatasnia ya habari wanafanya kazi kwa weledi, wizara imeunda kamati kutathimini uchumi wa vyombo vya habari.
Pia ametoa rai kwa waandishi wa habari wanawake wote nchini kujiunga katika chama hicho, kwa lengo la kukijenga na kuongeza nguvu zaidi.
Aidha alikipongeza Chama hicho kwa kuwajengea uwezo wanawake katika mambo mbalimbali, ikiwemo kupinga mila na desturi kandamizi.
Naye Mkurugenzi wa TAMWA Dk. Rose Reuben,amesema utafiti uliofanywa na TAMWA ndani ya vyumba vya habari 22, walibaini wahusika wengi wa unyanyasaji wa kijinsia ni watu wenye mamlaka ndani ya vyombo vya habari wakiwemo wahariri.
Pia amesema katika kuhakisha wanakabiliana na ukatili ndani ya vyombo vya habari, TAMWA inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Baraza la Habari Tanzania (MCT)
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe amesema wataendelea kutafuta fursa za ndani na nje ya nchi ili kujiinua zaidi na kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na asasi za kijinsia.
Amesema TAMWA kwa kushirikiana na asasi nyingine wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupitiwa kwa sheria ya makosa ya kujamiiana na kuanzishwa kwa sera ya jinsia katika vyombo vya habari, kuongezeka kwa nafasi za wanawke katika vyombo vya habari.
Aidha pamoja na mambo mengine katika mkutano huo TAMWA ilizindua ripoti ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia katika vyombo vya habari nchini.