DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro amesema Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea ombi la kujenga Makumbusho ya Mwami Ntare mkoani Kigoma na Makumbusho Maalum kwaajili ya kuenzi michango mbalimbali ya Wanawake walioshiriki katika ukombozi wa Taifa la Tanzania.
Waziri Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Aprili 13, 2024 wakati wa kilele cha kusherehekea mafanikio ya Mwami Tereza Ntare II ambaye alikuwa Chifu mwanamke wa kwanza katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam ambapo ameshiriki pia kuzindua onesho la historia ya Mwami Tereza Ntare litalakalodumu kwa mwezi mmoja.
“Kujengwa kwa Makumbusho hiyo utahifadhi historia sahihi kwa Taifa ambayo itakua imeandikwa na Watanzania wenyewe” amesisitiza Dk Ndumbaro
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Joseph Macha amesema Makumbusho ya Taifa iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanya utafiti na kukusanya mikusanyo itakayowezesha kuanzishwa kwa Makumbusho ya Mwami Ntare Tereza ili kuendelea kuenzi historia yake kwa manufaa ya jamii .
Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Rose Marandu- Women Fund licha ya kushukuru mchango mkubwa unaotolewa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kuhifadhi na kutafiti ameitaka jamii kuendelea kutoa elimu juu ya namna ya kumuwezesha mtoto wa kike ili aweze kutimiza ndoto zake kwa manufaa ya mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Familia ya Mwami Tereza Ntare II Agnes Shinganya ambaye ni mjukuu wa Mwami Ntare amesema ni dhamira ya muda mrefu ya familia ya Mwami kuanzisha Makumbusho ya Mwami Ntare mkoani Kigoma ili kuendelea kuhifadhi historia ya Mwami Ntare kwaajili ya kutunza historia yake kwa manufaa ya watu wa eneo la Heru juu -mkoani Kigoma na Tanzania kwa ujumla.