Serikali bega kwa bega na wakulima
SERIKALI itaendelea kuhakikisha mkulima anapata thamani halisi ya kile anachokizalisha shambani kupitia mazao mbalimbali.
Akizungumza mkoani Mtwara alipotembelea maghala ya kuhifadhia mazao katika wilaya mbalimbali ikiwemo zao la korosho, Katibu Mkuu wa Wizara wa Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah amesema siyo tu kupata thamani halisi bali wanahakikisha anakiuza kwa wakati na bila urasimu.
Amesema katika msimu wa mauzo ya zao la korosho mwaka 2023/24 umemalizika hivyo wanataka kufahamu mafanikio, changamoto zilizopatikana kwenye msimu huo ili ziweze kutatuliwa.
“Kama wilaya, mkoa na kama wizara tunajipangaje kwenda kutatua changamoto hizo, Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan lengo lake ni kuhakikisha sekta zinaweka mazingira wezeshi”
Aidha kitendo hicho cha kuja kutembelea maghala hayo ikiwa ni pamoja na kuangalia maendeleo ya mfumo wa stakabadhi ghalani, kuzungumza moja kwa moja na wananchi ili kujua kero zao mbalimbali zinazowakabili hatimaye serikali itakaa kuona namna ya kuwezesha yale yaliyoonekana kuwa ni kikwazo na mazuri kwa ujumla.
“Kuja saiti, kuja filidi tutakutana moja kwa moja na wananchi, tutapata kujua kero zao na mwisho kabisa serikali itakaa kuona namna ya kuwezesha yale yaliyoonekana kuwa ni kikwazo”amesema
Aidha, Katibu Mkuu huyo yuko ziarani mkoani humo ambayo ameanzia wilayani Nanyumbu kisha kuendelea Masasi, Newala, Tandahimba ambapo atapata fursa ya kutembelea baadhi ya maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali kwenye Wilaya hizo ikiwemo zao la korosho.
Baadhi ya maghala hayo ikiwa ni pamoja na ghala la Kenoshukuru lililopo mangaka wilayani Nanyumbu, Africian, chiona na mtandi yaliyopo wilayani Masasi, ghala kuu la Tanecu lililopo wilayani Tandahimba.
Hata hivyo amekagua ujenzi wa kiwanda cha ubanguaji wa korosho cha Tanecu Cashewnut Industry kilichopo kitangali wilayani Newala mkoani humo kinachogharimu zaidi ya Sh bilioni 3 chenye uwezo wa kubangua 3,600 elfu kwa mwaka.
Akiwa kiwandani hapo, Katibu Mkuu huyo amesema kama wizara wezeshi ya viwanda na biashara ni kuhakikisha uendelezaji wa viwanda ndani ya nchi lakini kile kinachozalishwa na viwanda hivyo ikiwemo korosho ziweze kupata njia sahihi ya kwenda kuuzwa katika maeneo mengine