‘Serikali haikusitisha vibali usafirishaji mazao nje’

Maindi

SERIKALI imesema haijasitisha utoaji wa vibali vya kusafi risha mazao ya chakula nje ya nchi kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Taarifa ya Wizara ya Kilimo kwa vyombo vya habari jana ilisema wizara haijasitisha vibali hivyo na kuutaarifu umma na wafanyabiashara wa mazao ya chakula.

“Wizara ya Kilimo inapenda kuutaarifu umma na wafanyabiashara wote wa mazao ya chakula kuwa haijasitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Advertisement

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara kwa kufuata taratibu zote za kisheria imeendelea kutoa vibali vya kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi kupitia mfumo wa utoaji vibali wa kielektroniki.

Katika kipindi cha kuanzia Agosti 27 hadi Septemba 7, mwaka huu wizara imetoa vibali vya mahindi, maharage, unga na mchele kwenda nje ya nchi vyenye jumla ya tani 37,450.

Ilisema Wizara ya Kilimo inawasisitiza wafanyabiashara wa mazao ya chakula kwenda nje ya nchi au kuingiza ndani ya nchi kufuata taratibu zilizowekwa.