Serikali: Hatuachi mtu bima ya afya kwa wote

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

SERIKALI imesisitiza kwamba hakuna Mtanzania yeyote atakayeachwa nyuma katika suala la bima ya afya kwa wote, huku ikisisitiza watu wote kujiunga.

Aidha, imesema sheria inayokusudiwa kutungwa ya bima ya afya kwa wote haitakuwa msahafu wala Biblia bali itafanyiwa marekebisho kwa kadri ya mahitaji.

Pia imewataka Watanzania wadundulize ili wawe na bima ya afya itakayowawezesha kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua kwa sababu gharama za matibabu ni kubwa.

Advertisement

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo jana akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano kati ya wizara yake na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika kwenye jengo la watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam jana.

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza Septemba mwaka jana, na unakusudiwa kusomwa kwa mara ya pili katika mkutano unaoanza Jumanne ijayo.

Ummy alisema sheria hiyo haitalazimisha yeyote kujiunga na bima kwa lazima. Hata hivyo, alisema  kutokana na umuhimu wake, Watanzania wote wanaombwa kujiunga kupunguza gharama za matibabu.

“Halitakuwa kosa kisheria (kutojiunga), kwa hiyo hakuna mtu yeyote atakayekamatwa, kuwekwa ndani au kufikishwa mahakamani,” alisema.

Ummy alisema bima ya afya si jambo rahisi, na mifano ya karibuni imeonesha namna nchi kama Marekani na za Ulaya zinavyohaha katika suala hilo.

Aliwaomba Watanzania kujiunga kwa wingi kwa sababu wingi wao ndio utakaofanya gharama za matibabu ziwe chini na hivyo wanufaika kuchangiana wenyewe kwa gharama nafuu zao.

Ummy alifafanua kuwa kwa mujibu wa muswada, kaya yenye watu sita ndiyo itakayohudumiwa na bima ambayo itaundwa na mwanachama mchangiaji, mwenza na wategemezi wasiozidi wanne, ambao mchangiaji atachagua mwenyewe wategemezi hao.

Alieleza kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa na za rufaa na zile za kanda, na pia imetoa fedha nyingi kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.

Katika wasilisho kwa wahariri kuhusu mambo muhimu ya muswada huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga, alisema mapendekezo ya awali ya huduma zilizofungamanishwa na upatikanaji wa bima ya afya zilikuwa tisa, lakini sasa zinapendekezwa kubaki tano.

Konga alitaja huduma zinazopendekezwa kubaki kuwa ni leseni ya udereva; bima za vyombo vya moto; leseni za biashara; viza kwa wageni na usajili wa wanafunzi wa vyuoni.

Alizitaja huduma zinazopendekezwa kuondolewa ni nne ambazo ni utambulisho wa mlipa kodi; usajili wa laini za simu; hati za kusafiri, usajili wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita; utoaji wa kitambulisho cha taifa.

Alifafanua kuwa utekelezaji wa ufungamanishwaji utafanyika kwa awamu kwa makundi ya kimkakati.

Aliitaja awamu ya kwanza (2023-2026) ambayo makundi yatakayofungamanishwa ni pamoja na wageni wanaoingia nchini na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Alisema awamu ya pili (2026-2028) itahusisha sekta isiyo rasmi kupitia leseni za biashara, udereva, bima za vyombo vya moto; na awamu ya tatu (2029- kuendelea) utakuwa ni utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kwa ulazima kupitia ufungamanishaji.

Konga alizitaja athari za kutokufungamanisha ni kushindwa kutekelezwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote na kutofikia lengo la afya kwa wote; wananchi kujiunga kwa hiari na wakiwa tayari ni wagonjwa na hivyo kuondoa dhana ya kuchangiana gharama za matibabu; na kudhoofisha uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya.

Alitaja manufaa yanayotarajiwa ni kundi kubwa la wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha; uboreshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba.

Manufaa mengine ni uhimilivu na ustahimilivu wa mfuko katika kutoa huduma, kuimarika kwa usimamizi na udhibiti katika utoaji wa huduma za bima ya afya zitolewazo na mifuko na kampuni binafsi za bima ya afya; kuboreshwa kwa vitita vya mafao vinavyotolewa na mifuko ya bima ya afya na kuimarisha hali ya kipato kwa wananchi.

Konga aliyewasilisha wasilisho hilo kwa niaba ya kikosi kazi cha kuandaa muswada huo, alisema chimbuko la kuandaliwa kwa muswada huo ni kutimiza wajibu wa serikali wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.

“Aidha, uhalisia unaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi (asilimia 85) hawana bima ya afya na hivyo kukosa uhakika wa kupata huduma za afya pindi wanapozihitaji, na sheria zilizopo kuweka uhiari wa wananchi katika sekta isiyo rasmi na sekta rasmi ya binafsi kujiunga na bima ya afya hatua ambayo inasababisha wengi kujiunga wakiwa tayari na matatizo ya kiafya,” alieleza Konga.

Aidha, alisema kutakuwa na kitita cha mafao ya huduma muhimu ambacho kila skimu ya bima ya afya italazimika kukitoa na kitakuwa haki ya kila mwanachama.

Alieleza kuwa kitita cha mafao cha huduma muhimu kitahusika na ada ya uandikishaji na kumuona daktari; gharama za vipimo; gharama za dawa aina zote (NEMLIT); na gharama za upasuaji mdogo na mkubwa.

Nyingine ni gharama za kulazwa; huduma ya afya ya kinywa na meno; huduma za matibabu ya macho; vifaa saidizi na huduma za mazoezi ya viungo.