Serikali: Hatuuzi, hatubinafsishi bandari
SERIKALI imesema hadi sasa haijapata kampuni ya kuwekeza katika bandari na haitauza au kubinafsisha bandari yoyote.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali za Tanzania na Dubai zimekubaliana kushirikiana kuendesha bandari na sasa wataalamu wanapanga na kuandaa mikataba ya uwekezaji itakayozingatia masuala kadhaa ukiwamo muda, gharama na maeneo ya kushirikiana.
“Hakuna bandari iliyobinafsishwa, hatutabinafsisha bandari, hatuuzi bandari, hakuna bandari iliyoko sokoni kutoka Tanzania, tunachotafuta ni kushirikiana na wawekezaji tuweze kuongeza ufanisi wa bandari zetu,” alisema Msigwa.
Aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma jana kuwa serikali ipo makini kulinda maslahi ya Watanzania hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwa kuwa inafanya hivyo pia kwenye sekta nyingine zikiwamo za madini, kilimo, usafirishaji wa majini na anga.
Msigwa alisema serikali haiwezi kukosa umakini wa kulinda maslahi ya Watanzania kwenye bandari kwa kuwa ni eneo muhimu na la kimkakati.
Alisema serikali ikipata mwekezaji katika bandari itawajulisha Watanzania na wananchi waelewe kwamba hakuna bandari iliyouzwa.
“Hata huo uwekezaji mpaka sasa nchi yetu bado hatujafunga mkataba wowote wa utekelezaji wa mradi wa uendeshaji wa bandari, mpaka sasa bado.
“Kwa hiyo wataalamu watakapokamilisha hayo majadiliano, tuangalie maslahi yetu yapo wapi, maoni yanayotolewa na Watanzania, kwamba tunataka iwe ya muda gani yatazingatiwa,” alisema Msigwa.
Alisema serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha bandari na hadi sasa hakuna mikataba ya kuendesha bandari.
“Tutakapokamilisha Watanzania tutawaambia kwamba sasa tumekubaliana kushirikiana na kampuni fulani, kuendesha bandari fulani, ama tumekubaliana na kampuni fulani kuendesha gati fulani kwa shughuli fulani, ama tumekubaliana na kampuni fulani kuweka mifumo hii na hii na itakuwa kwa muda gani, hayo yote mpaka sasa bado hayajafanyika,” alisema Msigwa.
Juzi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo alisema baadhi ya watu wanapinga uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu ya vita ya kiuchumi.
Chongolo alisema hayo mjini Kigoma wakati anatoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa serikali kusaini makubaliano na Serikali ya Dubai ili kampuni ya DP World ya nchini humo iwekeze katika bandari hiyo.
Alisema uwekezaji katika bandari hiyo utaiwezesha kuongeza ukusanyaji mapato kutoka trilioni 7.6 kufikia trilioni 26.7 sanjari na kupunguza gharama kwa meli kusubiri kushusha na kupakua shehena katika bandari hiyo.
Juzi Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana alisema Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kuuza bandari hivyo wananchi wawe watulivu kuhusu uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kinana alisema hayo katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mkendo uliopo Musoma mjini mkoani Mara na akasema serikali inapokea maoni kuhusu uwekezaji huo.
“Akauze bandari sababu ni ipi? Ili iweje? Ukisikiliza mjadala wote tunaotetea, wanaopinga, wanaokosoa hakuna anayesema kusiwe na uwekezaji hata mmoja, wote wanakubali kuna haja ya kuwekeza na lengo ni moja kuongeza ufanisi na kuongeza mapato,” alisema Kinana.