DC Rungwe aomba MeTL ibanwe mashamba ya chai

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

MKUU wa Wilaya ya Rungwe Dk Vicent Anney,  ameishushia lawama kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL), akidai inaua kilimo cha chai na ajira wilayani kwake.

Ametoa malalamiko hayo leo kwenye mkutano wa wadau wa zao la chai nchini unaofanyika mjini Iringa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, akiiomba serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru hali hiyo.

Alisema utafiti uliofanywa na wilaya yake unaonesha wakulima wadogo wilayani humo wanazalisha zaidi ya kilo 1,700 za chai kwa hekta moja, huku Kiwanda cha Wakulima Tea Company (Watco) kikizalisha zaidi ya kilo 2,200 kwa hekta moja.

Advertisement

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya huyo alisema hali ni tete katika shamba la MeTL wanaozalisha kilo 900 tu kwa hekta moja katika shamba lao lenye ukubwa wa hekta 1,150, ambalo hekta zake 500 haziendelezwi.

Alisema mwaka 2001 kampuni hiyo inayomilikiwa na bilionea Mohammed Dewji ilikabidhiwa shamba la Tukuyu Tea Estates lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 1150 na viwanda viwili vya chai ili viendelezwe.

“Naomba hili la Mohammed Enterprises lifanyiwe kazi. Hata hivyo viwanda viwili alivyokabidhiwa kimoja kimekufa kabisa, tunashindwa kuelewa malengo yake ni nini,” alisema.

Alisema kinachofanywa na MeTL wilayani humo kwa sasa ni kununua chai kutoka kwa wakulima wadogo, huku ikiwa haina mpango wowote wa kuendeleza shamba hilo na kuboresha viwanda hivyo ili kuchochea uzalishaji wa zao hilo.

Alisema hatua ya kampuni hiyo kutelekeza uwekezaji huo mbali na kuipotezea serikali mapato makubwa ya kodi na tozo mbalimbali, kumesababisha zaidi ya watu 1,000 waliokuwa wakifanya kazi wapoteze ajira.

“Kama kampuni hiyo haina mpango wa kuzifanyia kazi changamoto zake ili kurudisha uzalishaji naomba shamba hilo wapewe wananchi wangu, ili walime kuongeza uzalishaji wa zao hilo,” alisema.

Aliyekuwa Spika wa Bungela Tanzania, Anne Makinda alisema suala la MeTL wilayani Rungwe ni la muda mrefu na akaomba serikali iiongeze kasi katika kulifanyia kazi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *