‘Serikali isiongeze muda ujenzi soko Kariakoo’

DAR ES SALAAM; SERIKALI imetakiwa kutoongeza muda wa ujenzi wa Soko la Kariakoo kwa mkandarasi ili kuharakisha ujenzi wa soko hilo. Mradi wa soko hilo la kimataifa ulitarajiwa kukamilika Oktoba 2023 kabla ya kuongezwa muda mara mbili hadi Agosti 2024.

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ofisi ya Rais Tamisemi imesema Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia kutoa Sh bilioni 29 ili kukarabati soko la zamani na kujenga jipya litakalohudumia wafanyabiashara zaidi ya 3,000 huku likiwa na vizimba 975.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Justin Nyamoga alisema hayo jana mkoani Dar es Salaam kamati ilipohitimisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya soko hilo lililojengwa kwa mfumo wa kisasa wa kukabiliana na changamoto ya moto.

Advertisement

Alisema kamati imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi ambao umefika asilimia 93 .

Pia imeridhishwa na mpangilio wake utakaowezesha watu wengi kupata huduma ndani ya soko.

“Kamati inamtaka mkandarasi na wasimamizi wake kukamilisha mradi kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma…,” alisema.

Aliongeza, “Pia kamati imeielekeza serikali kuhakikisha wafanyabiashara wanaostahiki kuingia ndio waruhusiwe na kupewa nafasi na nafasi zitakazobaki zigawanywe kwa kufuata utaratibu shindani unaoangalia sifa stahiki,” alisema Nyamoga.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/ujenzi-soko-la-kariakoo-tayari-kumenoga/

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Zainab Katimba alisema kwa kuwa mkandarasi wa mradi tayari ameshaongezewa muda mara mbili, sasa ni mara ya mwisho na kwamba serikali haitaongeza tena.

Aliongeza kuwa serikali inategemea hadi kufika Mwezi Agosti mradi utakuwa umeanza kutumika kwa sababu wajasiriamali wamevumilia vya kutosha na sasa wanahitaji kuanza kufanya shughuli zao. “Tumewapa muda hadi kufika mwezi wa nane ili wananchi waanze kunufaika na soko hili lakini pia wafanyabiashara zaidi ya 3,000 na wenyewe waje waanze shughuli zao za ujasiriamali na kupata kipato,” aliongeza Katimba.

Katibu Tawala Msaidizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amani Mafuru alisema ukarabati na ujenzi wa soko jipya unaotekelezwa na mkandarasi Esteem Construction, ulitakiwa kukamilika Oktoba 2023 lakini akaongezewa muda hadi Aprili 2024 .

Mkandarasi alishindwa kukamilisha, akaongezewa hadi Agosti 2024.

Mjumbe wa Kamati, Eric Shigongo alitahadharisha uongozi wa soko hilo kuwa makini na ujio wa Soko la Kimataifa la Afrika Mashariki linalojengwa na Wachina Ubungo ili lisiue soko la Kariakoo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya soko hilo, Hawa Ghasia alisema uongozi utafanya kila liwezekanalo kuhakikisha soko la Ubungo halileti athari katika Soko la Kariakoo.