Serikali kuanzisha taasisi upasuaji ubongo
DAR ES SALAAM; Wizara ya Afya imedhamiria kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia masuala ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ili kuboresha huduma hizo za ubingwa na kutoa katika Taasisi ya Mifupa Ubongo (MOI) ambapo itabakia na masuala ya upasuaji wa mifupa pekee.
Waziri wa Afya. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Aprili 27, 2024 baada ya uzinduzi wa chama cha madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu kikiongozwa na Rais wa chama hicho Dk Othmani Kiloloma Jijini Dar Es Salaam.
“Lengo la chama hiki ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na salama za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, ikiwemo upatikanaji wa madaktari bingwa wa upasuaji ubongo na mishipa ya fahamu,” amesema Waziri Ummy.
Amesema Tanzania kuna madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu 25 tu, ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inapendekeza angalau katika kila watu 150,000 kuwe na daktari bigwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu mmoja.
“Ukichukua idadi ya madaktari bigwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu 25 tulionao maana yake kwa Tanzania daktari bigwa mmoja anahudumia Watanzania milioni 2,400,000, huduma hizi bado hazijawafikia Watanzania wengi ndio maana chama hiki kimekuja ili pia kujengeana uwezo na kuhamasisha madaktari wengine waweze kusomea fani hiyo ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu”,amesema Waziri Ummy.