Serikali kuchukua hatua dhidi ya biashara za watoto

SERIKALI imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa mashirika binafsi yaliyopewa dhamana katika uendeshaji wa makao ya watoto ,na nyumba salama endapo itabainika yanajihusisha na kufanya biashara ya watoto.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju ametoa tahadhari Desemba 10, 2022 wakati akifungua kikao kazi kati ya serikali na wadau wa Jukwaa la Kitaifa la Malezi mbadala ya watoto mjini Morogoro

Jukwaa hilo limeundwa na watendaji wa serikali na wadau wengine na kukutana kwa mara ya kwanza likiwa na kauli mbiu “ Familia Salama kwa Malezi , Makuzi na Maendeleo ya kila mtoto katika kufikia utimilifu wake “ ambalo lilizinduliwa na Kaimu Katibu mkuu huyo.

Advertisement

Mpanju amesema hadi sasa jumla ya mkao ya watoto 325 yamesajiliwa yakiwemo mawili ya Serikali yenye jumla ya watoto 9,011 kati yao wavulana ni 4,897 na Wasichana 4,114.

Kaimu Katibu mkuu huyo alisema si watu wote wanafanya jukumu hilo kwa nia njema , kwani kumekuwa na vitendo kwa baadhi ya makao na nyumba hizo watu wake wanajihusisha na biashara ya watoto kwa maslahi yao binafsi.

Hivyo amemtaka Kamishna wa Ustawi wa Jamii pamoja na wadau kuhakikisha makao ya watoto na nyumba salama zinazosajiliwa zinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo, kanuni na sheria za nchi.

“ Mtu asitumie mwanya huo kwa maslahi binafsi kwa sababu lengo la serikali ni kuhakikisha makao na n jia zote mbadala zinalenga kumlinda mtoto na kumwendeleza kwa kuzingatia maslahi mapana ya m toto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2019, kifungu cha 16 na 144” amesema Mpanju

Pia amemtaka Kamishna na watendaji wengine wa wizara hiyo ngazi za wilaya na mikoa kuhakikisha makao ya malezi mbadala yaliyopo katika maeneo yao yanafuatiliwa ili yasiwe sehemu ya manyanyaso kwa watoto ,kufanyiwa ukatili na wengine kugeuza kufanya biashara.

“ Fuatilieni makao haya na yanayobainika kwenda kinyume na sheria zilizopo ,makao hayo yafungwe mara moja “ amesema Mpanju.

Amemwagiza Kamishna kwa kushirikiana na Tamisemi kuhakikisha makao takribani 98 yaliyotambuliwa kuendesha shughuli zake bila leseni na yale bado kutambuliwa ,wamiliki wapewe utaratibu wa kiserikali wa namna ya kuyaendesha ili wauzingatie.

“ Mkiwapatia utaratibu huu wa kiserikali na kama hawataweza kuutekeleza makao hayo yafungwe mara moja na watoto waliopo watafutiwe makao yaliyo karibu nao wapelekwe yakiwemo ya serikali ambayo pia yana nafasi “ ameagiza Mpanju

Amesema kuwa ,serikali imeendelea kuratibu huduma ya malezi ya Kambo na Kuasili ambapo kwa kipindi cha 2020/21 Wizara ilipokea maombi 110.

Amesema jumla ya watoto 40 waliwekwa kwenye malezi ya kambo na watoto 50 waliasiliwa wakiwemo wakiume 28 na wakike 22 ikilinganishwa na maombi 131 ambapo jumla ya watoto 48 kati yao wakiume 21 na wakike 27 waliwekwa kwenye malezi ya kambo na watoto 56 waliasiliwa kati ya hao wakiume 17 na wakike 39 kwa mwaka 2021/22.

Ameiomba Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), kutumia mifumo madhubuti ya tehama, itakayosaidia kuweka takwimu sahihi kwa kuwabaini watoto wanaohitaji Malezi mbadala.

Mpanju amesema suala la Malezi Mbadala liwe ni suala la mpito, kwani anaamini kuwa kila mtoto aliye ndani ya Jamii ana mlezi wake hivyo Jamii isichululie suala la Malezi Mbadala kama ndio suluhisho la kudumu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *