NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wizara hiyo chini ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana, Dkt Doto Biteko itaendelea kusimamia miradi ya umeme kwa uaminifu mkubwa .
Kapinga amesema hayo mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk David Mathayo David iliyopofanya ziara ya kawaida kukagua utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 220 kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya Mwendokasi (SGR).
Naibu Waziri amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha kiasi cha Sh bilioni 76.23 zilizokamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 220 kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya Mwendokasi (SGR).
Amesema fedha hiyo imetukika kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme ya vituo vitakavyowezesha kulisha na kupoza umeme kwa kiwango cha kuendesha Treni hiyo kwa awamu ya kwanza (SGR lot 1) kutoka Kinyerezi Dar es Salaam hadi Kingolwira mkoani Morogoro yenye urefu wa kilometa 160 .
Vituo vya kupoza umeme vilivyojengwa ni cha Pugu, Ruvu, Kidugalo na Kingolwira ambavyo Mradi umeshakamilika kwa asilimia 100 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Amesema , serikali pia imetoa Sh bilioni 97.5 kwa awamu ya pili ya mradi huo wenye urefu wa kilometa 416 kutoka Msamvu mkoani Morogoro hadi Kintinku ( Manyoni ) mkoani Dodoma na kazi inafayika sambamba na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme cha Msamvu ( Morogoro) na Zuzu ( Dodoma).
Kapinga amesema , awamu hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vidogo saba vya kupoza umeme ufikie kiwango cha kutumika kwenye treni ambavyo ni Mkata , Kidete , Godegode , Igandu, Ihumwa , Kigwe na Kintinku ambapo kipande cha kutoka Msamvu hadi Ihumwa (SGR Lot 2-1) umefikia asilimia 99 ambao ulianza Oktoba 15, 2020 na unatarajiwa kukamilika Januari 31, 2024.