Serikali kuendelea umeme jotoardhi

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali imeamua kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha  nchi inazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wake.

Amesema chanzo hicho cha umeme kitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya maji na gesi asilia.

Dk Biteko amesema hayoleo mara baada ya kukagua vyanzo vya jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya akifuatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera.

Advertisement

” Miradi hii ya Jotoardhi sasa lazima ianze, tutaanza na megawati 10 hapa Kiejo-Mbaka na Ngozi tutaanza na megawati 30 huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine kama wa Jua  wa Kishapu (150 MW) ambao umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo ukiwemo wa  Makambako  na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi.” Amesema Dk Biteko

Aidha,amewaelekeza watendaji wa Kampuni ya Uendelezaji wa Joto Ardhi Tanzania  (TGDC) kufanya kazi zinazoleta matokeo  na si stori kwani Serikali inatafuta fedha za kutekeleza miradi hiyo na wajibu wa watendaji wa Taasisi hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.

Aidha Dk Biteko amesema kuwa,  Rais Dk Samia Suluhu Hassan anataka kuona watanzania wanapata huduma  bora katika sekta zote,  wanatolewa kwenye umaskini, anataka vitendo na siyo maneno, anataka kuona watu wahudumiwa na kufuatwa walipo, wanasikilizwa shida zao na kutatuliwa.

Ameongeza kuwa, Rais, Dk Samia anataka utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali iangalie miaka mingi mbele na si muda mfupi hivyo ametoa uhakika kwa wananchi kuwa miradi hiyo ya Jotoardhi itatekelezwa.

Pia,Kuhusu changamoto ya umeme, amesema kuwa, imetokana na vyanzo vya umeme nchini kwa muda mrefu kujikita  kwenye makundi matatu tu ambayo ni maji (570MW), mafuta na gesi  asilia.

Amesema kwa sasa, vyanzo vya umeme vinatokana na gesi asilia na maji ambavyo bado havitoshelezi mahitaji kutokana na kuzidi kukua kwa maendeleo, idadi ya watu kuzidi kuongezeka, miji kukua na umeme sasa kuwa ni hitaji muhimu.