Serikali kufanya utafiti mmomonyoko wa maadili

WIZARA ya Katiba na Sheria inatarajia kuunda timu itakayojumuisha wadau wa serikali na wa Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya utafiti kuhusu mmomonyoko wa maadili.

Pia wizara ina mkakati wa kuimarisha maeneo matatu ya sekta ya sheria ambayo ni usuluhishi, uandishi wa miswada ya sheria na majadiliano ya mikataba.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema hayo Dodoma jana wakati anafungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dk Ndumbaro alisema inaundwa kamati kutekeleza maelekezo ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye ameiagiza serikali ifanye utafiti kujua ukubwa wa tatizo la mmomonyoko wa maadili.

Alisema alipokea barua ya Bunge ya kuitaka serikali ifanye utafiti kuhusu suala la mmomonyoko wa maadili na amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo aunde timu ya kushughulikia suala hilo.

“Sasa hivi kuna malalamiko mengi sana na Mheshimiwa Spika (Dk Tulia Ackson) alitoa mwongozo au maelekezo kwa serikali kwamba serikali ifanye utafiti wa mmomonyoko wa maadili ambao unapelekea ongezeko la makosa dhidi ya maadili.”

“Jana (juzi) nimepokea barua hiyo na nimemwelekeza Katibu Mkuu aunde timu itakayoshirikisha wadau wote wa serikali Tume ya Mabadiliko ya Sheria kufanya utafiti huo.”

Dk Ndumbaro alisema kuanzia sasa hakuna sheria mpya itakayotungwa au kufanyiwa marekebisho bila kufanyiwa utafiti.

Aidha, alisema pia wizara ina mkakati wa kuimarisha maeneo matatu ya sekta ya sheria ambayo ni usuluhishi, uandishi wa mikataba na majadiliano ya mikataba.

Dk Ndumbaro alisema serikali haina mpango wa kuifuta Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na badala yake itaiimarisha kwa kuifanyia mabadiliko sheria.

Aidha, aliwataka wajumbe wa baraza hilo watumie baraza kwenye mambo ya msingi, yenye tija na yenye maslahi kwa wafanyakazi wote na si kuwa chanzo cha vurugu na kuwa jukwaa la kuleta migongano, fitina na uchochezi.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alisema baraza hilo lina kazi ya kupokea na kujadili mpango wa bajeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2023/24.

Alisema maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuishauri serikali masuala ya kisheria, kuandaa toleo la sheria ndogo zilizorekebishwa mwaka 2023 ambapo wamepitia sheria ndogo 18,000.

Habari Zifananazo

Back to top button