WAZIRI wa Uwekezaji , Viwanda na Biashara , Dk Ashatu Kijaji amesema serikali imedhamiria kuona viwanda vyote nchini vinafanya kazi kwa siku zote saba za wiki na hakuna kitakachofungwa kwa kushindwa kujiendesha kutokana na masharti ya uwekezaji au kukosa masoko ya bidhaa wanazozalisha.
Kijaji alisema hayo lipotembelea kiwanda cha 21 st Century Textile LTD kilichopo eneo la Kihonda viwandani katika Manispaa ya Morogoro.
“Niseme kwanza hakuna kiwanda kitakachofungwa katika serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan…Vingine vilivyofungwa vitaanza kufanya kazi tukianza na kiwanda cha nguo cha mkoani Mara, ” alisema Dk Kijaji.
Alisema Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 imeitaka serikali kuendeleza viwanda vilivyopo na kufufua vilivyokufa ili kuweza kutengeneza ajira za Watanzania milioni nane.
Dk Kijaji alisema serikali inawahitaji wawekezaji kuongeza uzalishaji na kutoa ajira zaidi kwa watanzania kikiwemo kiwanda hicho ambacho zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wake ni wanawake .
Alisema serikali ipo tayari kushirikiana na kiwanda hicho kutatua changamoto mbalimbali zilizowasilishwa zikiwamo kukatika mara kwa mara kwa umeme na maji .
Waziri Kijaji alisema hatua nyingine ni kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za nguo kinyemela nchini bila kulipa kodi na kuleta ushindani wa kibiashara baina yao na viwanda vya nguo nchini kikiwamo cha 21st Century .
Dk Kijaji aliwataka wenye viwanda watumie kuzalisha nguo zao katika ubora wa viwango vya soko la kimataifa. Alisisitiza kuwa serikali imeweka mazingira mazuri kutumia soko huru la Marekani kutokana na juhudi za Rais Samia.
Meneja wa Utumishi na Utawala wa Kiwanda hicho, Nicodemus Mwaipungu, akitoa taarifa za utekelezaji wa kiwanda hicho alisema hadi sasa kimetoa ajira za kudumu zaidi ya 2,400 kwa Watanzania.
Mwaipungu alisema lengo lilikuwa ni kufikia ajira 3,000 lakini kutokana na changamoto za maji, umeme pamoja na ushidani wa kibiashara unaosababishwa na uingizwaji kinyemela wa bidhaa nchini bila kulipia kodi, hakikukidhi lengo hilo.
Aliomba serikali kusaidia kupambana na waingizaji haramu wa bidhaa za nguo ambao wamekuwa wakiuza kwa bei ndogo na kusababisha kiwanda hicho kutofanya bishara iliyotarajiwa.
Mwaipungu alisema kiwanda kinatarajia kuongeza ajira nyingine 1,400 baada ya kukamilika kwa upanuzi matumizi ya teknolojia za uzalishaji nguo hasa fulana na aina nyingine .