Serikali kufunga kamera barabarani kudhibiti ajali

SERIKALI ina mpango wa kuja na mfumo mpya wa kufungwa kamera katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia magari yote na kubaini mwenendo mzima wa uendeshaji barabarani.

Mfumo huo utaunganishwa na Mfumo wa Mwenendo wa Mabasi (VTS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) pamoja na polisi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Latra, Profesa Ahmed Mohamed alisema hayo mkoani Dar es Salaam jana wakati mamlaka hiyo ikikabidhi vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi nchini ambavyo ni kompyuta tano na luninga mbili zitakazowekwa makao makuu ya polisi nchini na nyingine eneo la Msamvu, Morogoro.

Advertisement

Kuhusu mfumo mpya, Profesa Ame alisema serikali iko katika mchakato wa kutekeleza mfumo huo mpya ambao ni kamera za barabarani na utafanya kazi na mfumo wa VTS.

“Mfumo huo utaongeza usalama na kukabiliana na ajali za barabarani,” alisema Profesa Ame. Kuhusu vifaa vilivyokabidhiwa alisema vitalisaidia Jeshi la Polisi kufuatilia mwenendo wa mabasi hususani yale yanayokwenda masafa marefu. Alisema Latra imeona kuna umuhimu mkubwa kushirikiana na polisi, lengo likiwa ni kuwaongezea uwezo kwa kuwa sasa usalama barabarani si mzuri na ajali zimekuwa zikigharimu maisha na mali za watu.

“Mabasi yamekuwa yakiendeshwa kwa kasi kuliko mabasi ya kasi yenyewe, pia wapo madereva wanaochezea mfumo wa VTS,” alisema Profesa Ame na kuongeza kuwa lazima madereva wanaofanya hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria na hata wale wanaokwenda kinyume na utaratibu wa usafiri.

Aliitaka polisi kutumia vyema vifaa hivyo kwani vimenunuliwa na wananchi na gharama yake ni Sh milioni sita.

Naye Kamanda wa Polisi, Meloe Buzama alisema mpango mpya wa kamera utasaidia kuonesha dereva anavyoendesha na akikosea anachukuliwa hatua.

Alisema hivi sasa wanatafuta mawakala wa kuleta vifaa vitakavyotumika na vitafanyiwa majaribio kuona utendaji wake. Mkurugenzi wa Latra, Habibu Suluo alisema mfumo wa VTS una uwezo wa kuona basi lilipo na kutoa taarifa kwa polisi.

Alisema mfumo huo unapunguza ajali barabarani na unaokoa maisha ya watu wengi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *