Serikali kuimarisha ubora wahitimu uhandisi UDSM

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Jakaya Kikwete amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, inatekeleza mradi unaolenga kuongeza idadi na ubora wa wahitimu wa elimu ya uhandisi katika chuo hicho.

Dk Kikwete amesema hayo jana katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia, tukio lililofanyika katika ukumbi wa maktaba mpya chuoni hapo.

Akizungumza kwa niaba ya Rais huyo mstaafu, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwanaidi Maajar amesema kumekuwa na malalamiko hivi karibuni kutoka kwa waajiri kuhusiana na ubora na viwango vya utendaji vya wahitimu wa mafunzo ya uhandisi wakidai kuwa wanapofika eneo la kazi hasa viwandani kila kitu huonekana kipya na huwa kama wanaanza upya mafunzo.

Maajar alisema kuwa Changamoto hiyo inawezekana inachangiwa na mambo mawili, moja mtaala unasisitiza nadharia zaidi na kusahau vitendo, lakini mtaala huenda umepitwa na wakati.

“Tumeshaeleza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni wakongwe katika elimu ya juu nchini na cha kwanza kutoa wahitimu wa digrii ya uhandisi. Msisitizo hapa ni kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina jukumu kubwa la kuchukua katika kuhakikisha kuwa wahitimu wetu wanaendana na mabadiliko ya teknolojia na mwenendo wa soko.” Amsema Maajar, kwa niaba ya Dk Kikwete.

Amefafanua kuwa miongoni mwa juhudi za zinazofanywa kuondokana na changamoto hiyo ni pamoja na idara mbalimbali za Serikali kunufaika kupitia mradi wa Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye tija (ESPJ) uliomalizika hivi karibuni uliolenga kuongeza ubora wa wahitimu.Maajar aliongeza kuwa mradi wa elimu ya juu kwa mabadiliko ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation–HEET) unakusudiwa kuongeza umuhimu wa programu za shahada mbalimbali kuzioanisha na soko la ajira kwenye mradi wa HEET, uhandisi ni kati ya maeneo ya kipaumbele na katika matokeo chanya ya kutoa taaluma ya uhandisi.

Katika kuboresha miundombinu ya chuo hicho, Majaar alisema chuo kitatumia sehemu ya fedha ya mradi huo kuboresha miundombinu na kuboresha nyenzo na vifaa vya kujifunzia.

Alisema matumaini yake kwamba maboresho hayo pia yatajumuisha uwekezaji ndani ya Ndaki ya Uhandisi na taaluma zingine zinazohusiana na uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sherehe za maadhimisho hayo yalianza juzi Mei 16, ambapo yalihitimishwa jana Mei 17, 2023 katika eneo la maktaba mpya chuoni hapo.

Habari Zifananazo

Back to top button