Serikali kuja na bajeti rasmi barabara zilizoharibiwa

DODOMA; SERIKALI imesema wakati wa bajeti kuu itakuja na tamko la bajeti mahususi kurejesha barabara zilizoharibiwa na mvua.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi bungeni mjini Dodoma leo Mei 30,2024 na kueleza kwa kuanzia wataleta bajeti mahususi kwa ajili ya barabara zilizoharibika kutoka na mvua zilizonyesha maeneo mbalimbali nchini na serikali itakuja na tamko rasmi kuhusu suala hilo.

“Niwapongeze waheshimiwa wabunge tunajadili bajeti ya ujenzi kipindi ambacho madaraja yameharibika sana na mvua ambazo zinaendelea.

“Niwapongeze wabunge kwa kuwa wameitendea haki bajeti hii, wamewatendea haki Watanzania kwa sababu wamejadili na wameonesha uhitaji wa kurekebebisha barabara zilizoharibika…Sisi serikali tumepokea hoja hizi ambazo wabunge  wamezisema…

“Moja imeongelea nyongeza ya bajeti hata sisi serikali tunauona uhitaji huo na uhitaji haupo tu kwenye nyongeza ya ukubwa bajeti…

“Kuna bajeti ambayo inahitaji marekebisho tu ya barabara zilizoharibika, tunalifanyia kazi hilo… Tunatarajia tutakavyokuja kwenye bajeti kuu tutatoa tamko kuhusu bajeti ya dharura mahususi kuhusu kurejesha barabara zilizoharibika,” amesema Waziri Nchemba.

Amesema walipokaa na Wizara ya Ujenzi walielezwa kuwa wanahitaji kwa barabara za ujenzi tu kati Sh bilioni 700 hadi Sh trilioni moja, wakati kwa Tarura wanahitaji Sh bilioni 300, hivyo watakuja na tamko hilo kwa ajili ya kurejesha miundombinu hiyo kwani uwekezaji uliofanyika ni karibu Sh trilioni 40, hivyo haiwezi ikaacha tu.

Pia imesema itakuja na pendekezo la kuanzisha chanzo kipya mahususi kushughulikia masuala ya dharura kwa ajili ya miundombinu iliyoharibiwa.

“Kuhusu upatikanaji wa fedha tutaleta pendekezo la chanzo kipya, Bunge lako litupitishie chanzo kipya mahususi, ambacho kitaenda kuongeza kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi na tutaangalia kianze kutumika mwaka huu na miaka mingine kitumike kama chanzo kwa masuala ya dharura,” amesema Waziri Nchemba.

Habari Zifananazo

Back to top button