Serikali kujenga mabwawa 14 

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo inatarajia  kujenga mabwawa 14 kwa ajili ya kuwezesha kilimo cha umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde leo  Oktoba 29,  2022 akiwa Gairo mkoani Morogoro katika maadhimisho ya wiki ya mkulima
Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Mavunde amesema kuwa dhamira ya Rais  Samia Suluhu Hassan ni kumfanya mkulima kuwa na uhakika na kilimo chake badala ya kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu kulima huku akisubiri mvua.
Na ndiyo maana, ameongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 hadi shilingi bilioni 954, ambayo kiasi kikubwa imeelekezwa kwenye ujenzi wa mabwawa na miundombinu ya umwagiliaji.” Amesema
Ameyataja mabwawa  hayo kuwa ni  Membe (Chamwino-Dodoma), Msingi (Singida), Kasoli (Simiyu), Katunguru (Mwanza), Iyombo (Tabora), Goweko, Nyida (Shinyanga), Ibanda (Geita), Luiche (Kigoma), Igwisi (Tabora), Kalupale (Tabora), Msagali (Mpwapwa-Dodoma),Mwamabondo na Tlawi (Manyara).
Aidha, amesema Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafanya mapitio ya mabonde yote makubwa nchini yapatayo 22 kwa lengo la kuyafanyia usanifu ili kuwezesha kujenga mabwawa makubwa ya umwagiliaji.
“Serikali haipo tayari kuona mkulima anateseka kuanzia mwanzo anapoandaa mashamba mpaka anapoyauza, ndo maana imeweka mkakati wa kumsaidia katika upatikanaji wa pembejeo na masoko ya mazao anayozalisha.”, Amesema
Amesema serikali imeleta ruzuku ili mkulima apate nafuu ya bei. Mbolea iliyokuwa iuzwe shilingi 140,000 sasa mkulima anainunua kwa elfu 70,000 pekee.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Gairo,  Jabir Makame, ameishukuru serikali kwa mikakati lukuki inayoitekeleza kwenye sekta ya kilimo, na kuahidi kuwa Wilaya ya Gairo ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo na kubainisha kuwa, kuanzia msimu ujao wa kilimo wamepanga kulima ekari 50,000 za alizeti.

Habari Zifananazo

Back to top button