Serikali kujenga nyumba 101 waathirika Hanang

DAR ES SALAAM: SERIKALI inatarajia kujenga nyumba 101 kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya matope yaliyotokea Halmashauri ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara Desemba, mwaka jana.

Kaya 1,150 zenye watu 5,600 zimepoteza makazi yake katika eneo la Katesh na maeneo yanayozunguka Jorodom, Ganana, Katesh, Dumbeta, Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi kutokana na maporomoko hayo yaliyosababishwa na miamba ya mlima Hanang kunyonya maji na hivyo kumeguka.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema serikali imetenga ekari 100 kwa ajili ya makazi hayo mapya baada ya kupata eneo lililokuwa shamba la Waret kutoka kwa Jeshi la Magereza.

Alisema eneo hilo lipo kwenye Kijiji cha Gidagamowd, Kata ya Mogitu wilayani Hanang ambalo ni umbali wa kilomita 4.5 kutoka barabara kuu ya Babati- Singida.

“Serikali mpaka sasa imesafisha eneo hilo na imepima viwanja 269 ambapo kati ya hivyo, 226 vya makazi pekee, 26 makazi na biashara, 17 eneo la huduma za kijamii kama zahanati, eneo la kuzikia, kiwanja cha michezo, eneo la wazi, majengo ya ibada viwanja vitatu, ofisi ya kitongoji moja, soko moja na shule ya msingi moja,” alisema.

Matinyi alisema serikali iliangalia nyumba zilizozolewa na zilizoharibika kwa kuingia tope na ndizo zilizopewa kipaumbele katika kupewa misaada.

Alisema serikali pia ilifanya ukaguzi kwa kutumia satelaiti kupita eneo la maafa na taarifa za sensa ya watu na makazi pamoja na zilizopo serikali ya mitaa na kujiridhisha ni nyumba 89 ndizo zilizozolewa kwa maporomoko hayo, na katika eneo lililokuwa hatarishi ambalo si eneo la kufanya makazi au shughuli za kiuchumi, kuna nyumba 12.

“Hivyo jumla ya nyumba zinazohitajika ni 101 ambazo serikali imechukua jukumu la kuwasaidia wananchi kujenga kuanza makazi mapya…lakini pia serikali imetenga viwanja vingi ili kuweka eneo la akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye au likitokea tatizo lolote,” alisema.

Alisema hatua inayofuata ni umilikishaji viwanja hivyo kwa wahusika ambavyo zitajengwa nyumba za vyumba vitatu na kuna ukamilishaji wa ubunifu wa ramani za nyumba na hesabu za gharama kisha kuanza ujenzi ambao lengo ni kutumia miezi mitatu kuanzia Januari hii.

Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea wananchi wa eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana aliahidi serikali itagharamia makazi mapya kwa ajili yao.

Kuhusu shule zinazotarajiwa kufunguliwa keshokutwa alisema, wanafunzi wote katika eneo lililoathirika watakwenda shule na kila kitu kimewekwa sawa kuanzia madarasa, sare za shule na vifaa.

“Hivi ninavyozungumza hapa Mkuu wa Mkoa wa Manyara (Queen Sendiga) leo (jana) anamaliza zoezi la kugawa vifaa kwa wanafunzi hao,” alisema.

Alisema katika maafa hayo serikali iligharamia vifaa mbalimbali vya tiba pamoja na chakula na huduma nyingine muhimu za binadamu ambapo mpaka sasa imetumia Sh bilioni 3.6 kutoka kwa wahisani mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa na klabu za mpira na kwamba bado misaada inaendelea kutolewa.

Matinyi alisema serikali kupitia mfuko wa taifa wa maafa kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliendelea kupokea fedha mpaka sasa ina Sh bilioni 2.7.

“Fedha hizo zikijumlishwa na fedha ambazo Rais alirejea nazo kutoka Dubai alipokwenda kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Sh bilioni 2.5 zinafika kama Sh bilioni 5.2,” alisema.

Katika maafa hayo watu 89 walikufa na 139 walijeruhiwa ambapo serikali iligharamia matibabu na mazishi ya watu 88 huku mwili mmoja wa mtoto ukiwa haujatambuliwa hivyo inafanya utaratibu wa kupima vinasaba kwa wanaohitaji ili kupata ndugu wa mtoto huyo.

“Mpaka sasa kuna majeruhi wanne, mtu mzima mmoja na watoto wa kike wawili katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Manyara, Babati na mtoto mmoja wa kiume yuko Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma,” alisema.

Taarifa ya serikali kuhusu chanzo cha maporomoko hayo ilisema ni sehemu ya mlima Hanang iliyokuwa dhoofu ilinyonya maji na kusababisha maporomoko na hivyo kusababisha tope ambapo sehemu iliyonyonya maji ilizua mkandamizo na sehemu ya mlima kushindwa kuhimili na kusababisha kumeguka na kutengeneza tope lililoanza kuporomoka kufuata mkondo wa mto Jorodom huku likizoa mawe na miti na kwenda kushambulia makazi ya binadamu yaliyo pembezoni mwa mto huo.

Habari Zifananazo

Back to top button