Serikali kujenga Sekondari Mahomanyika

SERIKALI kujenga sekondari katika eneo la Mahomanyika ili kuwapunguzia mwendo wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufuata shule katika eneo la Nzuguni wakitokea Mahomanyika.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika Mtaa wa Mahomanyika.

Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais  Samia Suluhu Hassan imepanga kutekeleza ujenzi wa shule ya Sekondari ya Mahomanyika ili kuwapunguzia mwendo watoto wa shule ambao kwa sasa wanatembea umbali mrefu kufuata sekondari katika eneo la Nzuguni.

Ujenzi wa shule hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kusogeza huduma hii ya elimu kwa jamii ili watoto wa shule wasitembee umbali mrefu.

“Ni matumaini yangu kwamba ujenzi huu ukikamilika utasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga sekondari na kuongeza ufaulu pia.”Amesema Mavunde

Katika mkutano huo Mavunde alipokea na kuzijibia hoja mbalimbali za wananchi likiwemo suala la ardhi ambapo atakutana na Mkurugenzi wa Jiji pamoja na Idara ya Mipango Miji ili kuziwekea utaratibu mzuri wa utatuzi wake.

Awali Diwani wa Kata yq Nzuguni  Alloyce Luhega  amemshukuru  Mavunde kwa kusaidia upatikanaji wa wa mtambo wa kuchimba mtaro ili kusogeza huduma ya maji kwa wananchi pamoja na ukarabati wa viwanja vya michezo kwa kuweka magoli ya chuma.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini Charles Mamba amewataka viongozi wote wachaguliwa kuhakikisha wanatoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuitisha mikutano ya mara kwa mara kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Habari Zifananazo

Back to top button