WAZIRI wa Habari, Mawasiliano wa Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara inakadiria kukusanya Sh bilioni 150.7.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara bungeni, jijini Dodoma leo Mei 19, 2023 amesema fedha hizo zitatokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, tozo itokanayo na kuongeza salio la simu na usajili wa Magazeti.
Kwa kuongeza alisema maeneo mengine wanayotarajia kukusanya fedha hizo kutoka katika ada ya mwaka ya Magazeti, vitambulisho vya Waandishi wa Habari na machapisho ya picha pamoja na mabango na majarida.
Aidha Waziri Nape amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuharakisha nchi kuelekea katika uchumi wa kidijitali hususan kuhimiza mfumo wa kufanya biashara bila fedha taslimu (cashless economy) ambao unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA.
“Ili kufanikisha haya kwenye Sekta zote za Uchumi na Kijamii, Wizara imepanga kufanya mabadiliko na maboresho makubwa kwenye Sekta ili kuendana na mageuzi haya ikiwemo kuharakisha ujenzi, uendelezaji na usimamiaji miundombinu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,” alisema waziri.
Aidha alisema wizara itafanya mapinduzi kwenye taasisi za sekta kwa kuimarisha mashirikiano na Sekta binafsi, kuendeleza tafiti na ubunifu kwenye masuala ya TEHAMA ikiwemo uanzishwaji na uendelezaji wa kampuni changa (startups), kuwezesha Sekta nyingine kuelekea kwenye mapinduzi ya kidijitali; na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.
“Wizara yangu itahakikisha Uchumi wa Kidijitali unawekewa mazingira bora ya kiudhibiti na kiuwekezaji ikiwemo kuandaa sera, miongozo na taratibu za kulinda maadili ya Kitanzania,” alisisitiza.