Serikali kulea ubunifu, sayansi kwa uchumi mkubwa

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (pichani) amesema kuwa nchi haiwezi kujenga uchumi bila kutoa kipaumbele kwenye ubunifu, sayansi na teknolojia.

Profesa Mkenda alisema hayo wakati wa kufunga maonesho ya Wiki ya Ubunifu yaliyofanyika jijini hapa na kusema kuwa: “Kama tunataka kujenga uchumi wa kitaifa hatuwezi kujenga uchumi kwa maneno, hatuwezi kuamini kuwa na mashamba mengi na ardhi yenye rutuba, tutashangaa tuna maeneo makubwa ya kulima ngano tunaagiza kutoka nje, tuna uwezo wa kuzalisha alizeti wenzetu wanazalisha vizuri kutokana na sayansi, teknolojia na ubunifu.”

Alisema pia serikali imetenga fedha kwa ajili ya watafiti watakaofanya utafiti utakaotambuliwa kimataifa kwenye maeneo ya sayansi na kila utafiti utakaokidhi vigezo utapewa Sh milioni 50.

“Tungependa kuona tafiti zinafanyika Sokoine kwenye mambo ya kilimo ni vipi tukilima alizeti Singida tunaongezaje uzalishaji kwenye ekari moja, sasa hivi hatuwezi kushindana na uagizaji mafuta kutoka nje kwa sababu tija yetu ipo chini,” alisema. Profesa Mkenda alisema hivi sasa Wizara yake imefanya juhudi za kujiunganisha na Diaspora kutoka nje ili kupata nafasi nyingi za kwenda kusoma.

Alisema nguvu kubwa itaelekezwa katika zile bunifu walizoona hapa na nyingine ambazo hawajaziona zinabiasharishwa, kwani ni muhimu kwa nchi. Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, baada ya kufanya maonesho hayo ya Makisatu zitapatikana bidhaa zilizoibuliwa, zimebiasharishwa na ni jukumu lao kuzitangaza.

Naye Katibu Mkuu, Profesa Carolyne Nombo alisema maadhimisho ya siku ya kilele cha ubunifu ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita katika kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema maadhimisho yaliambatana na maonesho ya teknolojia, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi za utafiti na maendeleo kutoka Vyuo Vikuu, Taasisi za kibiashara, Wakala wa biashara, Wizara, Taasisi binafsi na kampuni za teknolojia.

Tangu kuanzishwa kwa Makisatu mwaka 2019 jumla ya wabunifu na wavumbuzi wachanga wapatao 2,636 waliibuliwa na kutambuliwa na Wizara.

Habari Zifananazo

Back to top button