SERIKALI wilayani Ngara, imesema italinda mradi wa uchimbaji madini wa Tembo Nickel kwa wivu mkubwa ili kuhakikisha serikali na muwekezaji wananufaika.
Ofisa Tarafa ya Nyamihaga, Dadley Baham, aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi, akizungumza kwenye kikao cha uzinduzi wa Kamati ya Kuhamisha Watu na Makazi (RWG) kilichofanyika katika Kata ya Rulenge, alisema mradi huo ni wakimkakati na unamanufaa makubwa kwa taifa.
“Jambo kubwa hapa tunasisitiza juu ya uaminifu na uadilifu, Tembo Nickel na Serikali wanaushirikano maalum , kwahiyo kwenye kuzuia janja janja Serikali itakuwa na jukumu la kulinda masilahi yake yaliyo ndani ya mgodi huu na pia kumlinda mwekezaji.
“Kwahiyo msimamo wa Mkuu wa Wilaya yetu ni kuwa lazima tutalinda huu mradi kwa wivu mkubwa,”alisema. Aliwataka viongozi wa vijiji na madiwani, kuhakikisha wanakuwa daraja la kuelimisha wananchi juu ya mambo mbalimbali ikiwamo zoezi la uthaminishaji aridhi na mali linaloendelea kwa sasa. “Jukumu letu ni kuhakikisha mnakuwa waaminifu na daraja baina ya wananchi, mwekezaji na serikali.
Nyie ndo mnatakiwa kutoa uelewa pale kwenye upotoshaji, nyie ndo wa mnatakiwa kutusaidia kupeleka taarifa iliyo sahihi kwa wananchi wetu. Mlio hapa ni wawakilishi inamaana mmeaminiwa na wananchi, muwapelekee taarifa sahihi. “Sisi kazi yetu ni kuhakikisha haki inapatikana na maana ya kupata haki ni kwamba hakuna atakayeonewa,”alisema.
Kwa upande wa Meneja Usalama na Afya Kazini, wa Tembo Nickel Dk Kudra Mfaume, ambaye kwenye kikao hicho alimuwakilisha Meneja Mkazi wa kampuni hiyo, Benedict Busunzu, alisema lengo lao ni kuhakikisha mgodi unaanza uzalishaji robo ya kwanza ya mwaka 2026.
Alisema pia kabla ya kuanza kwa uchimbaji, kampuni itahakikisha kila mwananchi anayehamishwa ili kupisha eneo la mradi anapata fidia stahiki kwa kufuata sheria za Tanzania na kanuni za kimataifa (IFC) Alisema kuzinduliwa kwa RWG, kunatoa fursa ya majadiliano ya namna bora ya kuhamisha wananchi hao katika maeneo mengine.
Alisema zoezi la uthaminishaji linaloendelea kwa sasa linafuata sheria za Tanzania na kuzingatia kanuni za kimataifa ambazo masharti yake yapo juu zaidi . Kwa lengo la kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayestahili atapata fidia sitahiki.
Tarehe ya ukomo ya maendelezo ya kudumu kwenye eneo la mradi wa Tembo Nickel ilitangazwa, Julai 18 mwaka huu, na kwa sasa shughuli za uthaminishaji wa mali na ardhi unaendelea. “Picha za satelaiti zilishapigwa na kuonyesha kila kitu kilicho kwenye eneo la mradi, kwahiyo ni wanaostahili tuu ambao watapata fidia sitahiki,”alisema