Serikali kulipa tril 7.91/- deni la watoa huduma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande amesema serikali itahakikisha madeni ya Sh trilioni 7.91 wanayodai wafanyakazi na watoa huduma kwa mashirika ya umma yanalipwa na pia inadhibiti uzalishaji wa madeni mapya.

Hadi sasa, deni lililopo ni la Sh trilioni 7.91 na linajumuisha madeni ya wafanyakazi na watoa huduma kwa mashirika ya umma 71.

Chande alitoa kauli hiyo bungeni Dodoma Jumatano wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (Chadema) aliyetaka kujua ni lini serikali italipa madai ya Sh trilioni 7.91 ya watoa huduma kama yalivyoripotiwa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2021.

Advertisement

Chande alijibu ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa na kudhibiti uzalishaji wa madeni mapya, mashirika yote ya umma yameelekezwa kuandaa mkakati wa kukabiliana na madeni na kuwasilisha Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Katika mkakati huo, kila taasisi inatakiwa kuonesha namna itakavyodhibiti uzalishaji wa madeni mapya na kulipa madeni yaliyopo.  Lengo ni kuhakikisha kuwa kiwango cha madeni kinafikia asilimia mbili ya jumla ya bajeti ya mashirika ya umma ifikapo mwaka 2025.