Serikali kumaliza kero ya umeme migodini

GEITA: Serikali imeanza kutekeleza mradi maalum wa kupeleka umeme maeneo ya wachimbaji wadogo ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji na kuchagiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya madini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema hayo  wakati akizungumuza na wananchi baada ya kuwasha umeme katika vijiji vya Magenge na Kasesa, jimbo la Busanda wilayani Geita.

Dk Biteko amesema mradi huo ni sehemu ya miradi miwili inayotekelezwa wilayani Geita ambayo ni Mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA3R2) na mradi wa Kupeleka umeme migodini.

Amesema yapo malalamiko mengi ya wachimbaji wengi wadogo wakidai kutumia mitambo ya mafuta kuchimba na kuchenjua madini kwa gharama kubwa na hivo kuwa na faida na ufanisi mdogo.

“Kwenye wilaya hii ya Geita, ambapo Dhahabu inachimbwa kwa wingi, tunaleta umeme kwenye migodi midogo midogo kwa ajili ya wachimbaji wetu.

“Tunataka tupunguze gharama za uchimbaji kwa sababu bei ya mafuta inapanda kila siku, ni lazima tuwatafutie nafuu ya maisha wachimbaji wetu, na hii hatuzungumzi tu, tunazungumza jambo ambalo lazima litokee.”

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amekiri kwa sasa Mkoa wa Geita kuna uhaba wa nishati ya umeme maeneo ya visiwani lakini serikali imelitazama hilo na imekuja na mradi kuwafikia wakazi wa visiwani.

Mbunge wa Busanda, Mhandisi Tumaini Magesa amekiri iwapo umeme utafika maeneo ya wachimbaji wadogo itasaidia wachimbaji kuachana na teknolojia duni na kutumia teknolojia ya kisasa kuinua uzalishaji.

Awali Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema serikali imetenga  Sh bilioni 39.

1 kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme na hadi sasa vijiji 334 vina umeme kati ya vijiji 461.

Mhandisi Olotu amesema kwa Wilaya ya Geita pekee vijiji 70 vilikuwa bado havina umeme na wakandarasi wapo kazini na tayari Vijiji 42 vimeshapatiwa umeme na kazi inaendelea kuvifikia Vijiji vilivyosalia.

Taarifa ya Shirika la Umeme Nchini, (Tanesco) inaeleza Sh bilioni 18 zimetengwa kwa mradi wa Small Mining, kupeleka umeme maeneo 35 ya wachimbaji wadogo Mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu, Mara na Kagera.

Habari Zifananazo

Back to top button