Serikali kuondoa Ada vyuo vya ufundi

Fani ya afya, ufundi, sayansi, ualimu kupewa kipaumbele

SERIKALI imependekeza kuondolewa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa kujiunga na vyuo vya ufundi vya Dar es Salaam Institute of Teknology (DIT), Mbeya University of Science and Technology (MUST) na Arusha Technical College (ATC).

Hayo yamesemwa leo Juni 15,2023 Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba  akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya Wataalamu wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda .

Amesema, kufuatia mabadiliko ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, toleo la Mwaka 2023 na mabadiliko ya mitaala yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,  Serikali inalenga kutoa elimu ya amali kwa ngazi zote kuanzia shule za awali, elimu ambayo itamuwezesha kijana wa kitanzania kujiajiri au kuajiriwa na hivyo, kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa.

“Hivyo, napendekeza kuanzisha programu ya mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa na Serikali kusoma kwenye vyuo vinavyotoa elimu katika fani za kipaumbele ambazo ni sayansi, afya, ufundi na ualimu.”Amesema

Amesema hatua hiyo itaanza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo wa 2023/24.

ELIMU BILA ADA

Wakati huo huo, Mwigulu amesema pia, programu ya Elimumsingi na Sekondari bila ada imeendelea kuboreshwa ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imetekeleza jambo la kihistoria kwa kuwafutia ada wanafunzi wa kidato cha tano na sita na kuwafanya wanafunzi hao kusoma kwa utulivu.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia Programu hiyo ambapo hadi Aprili 2023 jumla ya shilingi bilioni 661.9 zimetolewa.

Vilevile, Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.41 kwa wanafunzi wa elimu ya juu na pia imeendelea na maboresho ya miundombinu ya vyuo ikijumuisha vyuo vikuu, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vya maendeleo ya wananchi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button