Serikali kuondoa changamoto ya sukari

SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa hadi kufikia Februari 15, 2024 changamoto ya upatikanaji wa sukari nchini itakuwa imepungua huku ikisisitiza kuwa bei elekezi ya sukari ni Sh 2700 hadi 3200 hivyo wafanyabiashara wanaopandisha bei wameanza kukamatwa.

Imesema inaendelea kuchukua hatua ili kudhibiti tatizo la bei ya sukari nchini ikiwemo kuruhusu uagizaji wa shehena ya kwanza ya sukari kutoka nje ya nchi yenye tani 500,000 ili kuondoa changamoto hiyo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alieleza hayo jana alipozungumza na wakazi wa Arusha kwa njia ya simu baada ya kupigiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda ambaye yupo ziarani mkoani humo na akamtaka aelezee hali ya halisi ya sukari nchini na sababu za bei kupanda.

“Nataka niwaombe Wananchi watulie na niwahakikishie kwamba Serikali imechukua hatua na niwaombe radhi kwa taharuki iliyojitokeza kutokana na viwanda vyetu kuathirika kwenye uzalishaji tumeamua kuagiza sukari kutoka nje na shehena ya kwanza inaanza kuingia kuanza Januari 26 hadi 30, 2024,” alisema Bashe.

Alisema wametoa vibali laki moja vya uingizaji wa sukari nchi.

“Nataka niwaambie Watanzania wote kupitia mkutano wako kwamba mpaka Februari 15, 2024 hali ya utulivu ya upatikanaji wa sukari itakuwepo na sio kwamba nchini hakuna sukari bali kuna tabia ya wafanyabiashara ambao tumekuwa tukiwalinda kwa muda mrefu kutengeneza upungufu usio halali, tumewakamata Watu wote ambao wanauza sukari zaidi ya bei elekezi na bei elekezi ya Serikali haitotakiwa kuzidi kati ya sh 2700 mpaka sh 3200 kwa nchi nzima,” alisema.

Bashe aliwaomba wakuu wa wilaya na wakuu wa mkoa huo wakishirikiana na Bodi ya Sukari kufanya tafiti katika maeneo yote yanayouzwa sukari kwasababu serikali haitamani kuona sukari inauzwa 4000.

“Jana imefanyika oparasheni katika maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza na wale watu ambao wamebainika kuuza sukari mpya nje ya bei elekezi ya serikali tumeshawakamata na tunatarajia kuwapeleka Mahakamani,” alisema.

Alieleza kuwa tayari wameshawaambia wazalishaji wa ndani kuwa serikali haitasita kuondoa sera ya kuwalianda wawekezaji wa ndani kama wawekezaji hao wanapata nafasi ya kulindwa kuwaumiza walaji wa mwisho.

Alisema wanaviwanda saba vya uzalishaji wa sukari ambavyo vinalindwa na serikali ndio maana wamekuwa wakiwaambia kuwa ni lazima waheshimi nafasi wanayopewa na serikali.

Alibainisha kuwa hali ya upungufu wa sukari nchi ulishawahi kutokea Mwaka 2018 hadi 2019 na serikali ilichukua hatua hizo hizo ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Kuhusu kero ya wananchi zaidi ya 2000 kukosa ajira baada ya mashamba saba ya maua kufungwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alipopigiwa simu na Makonda alisema watafuatilia na Waziri wa kilimo ili kuwapa wawekezaji sahihi watakaoendesha mashamba hayo bila kuyafunga.

Mkumbo alisema kila mwananchi waliokuwa wakifanya kazi katika mashamba hayo na wanadai watapewa kipaumbele ili wakati wa utoaji wa ajira pamoja na kusimamia ili walipwe fedha zao kwasababu bado wanashirikiana na wawekezaji na wameshaanza taratibu za kuandaa malipo ya fidia za wananchi.

Aidha Naibu Waziri wa madini, Steven Kiruswa alisema amepokea changamoto ya maboresho ya sheria ya madini ya Tanzanaite ambayo yananchimbwa Mererani lakini sheria ina sema wauziwe wageni pekee.

Alisema watawasiliana na mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Madini ili kujua kama sheria hiyo imeshaanza kufanya kazi kwasababu walifanya maboresho ya sheria hiyo na inatakiwa ianze kufanya kazi kuanzia Januari 28, Mwaka huu.

Makonda alimpigia simu Waziri wa Maji Juma Aweso baada ya kuambiwa na Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo kuwa wakazi wa Arusha wanakumbwa na changamoto ya bili za maji kuwa kubwa kwasababu watu wanaopita kusoma bili wanaongeza ela.

Aweso aliwataka wasoma mita kutosoma bili za maji bila kushirikisha wananchi pia aliahidi kufika mkoani hapo kutembelea vyanzo vya maji ili kubaini uwepo wa chumvi katika maji hayo.

“Si ruhusa msoma bili za maji kusoma mita za maji bila kushirikisha mtumiaji nitakuja Arusha kukagua vyanzo vya maji ili kubaini changamoto hii na kuitatua,” alisema Aweso.

Pia alisema wataongeza nguvu ili kuhakikisha wananchi wote wanapata mita za maji za ruku.

Habari Zifananazo

Back to top button