Serikali kupanua uhuru wa habari

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mabadiliko katika Sheria ya Huduma za Habari yamekuja kukuza sekta ya habari kwa kiwango kikubwa.

Majaliwa ameyasema hayo leo Machi 27, 2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, katika kilele cha Kurasa 365 za Mama, ikiangazia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

Amesema, licha ya uhuru uliopo katika sekta ya habari kwa kutoa maoni na kwamba sera imebana haijafungua milango ndio maana dhamira ya serikali ni kuendelea kufanya maboresho ya sera ili kuwe na sheria na kanuni rafiki katika kuendesha masuala ya habari nchini.

Advertisement

“Mageuzi haya yamewezesha jamii yetu kupata habari, sekta binafsi kuendesha vyombo vya habari, tunaona mkakati sasa ambao tunataka kuenda kupanua wigo zaidi wa mifumo ya watu kuanzisha vyombo vya habari,” amesema Majaliwa.

Kauli ya Majaliwa imekuja ikiwa ni miezi 11 tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha mabadiliko hayo ya Sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016, Juni 13, 2023.