Serikali kupata mwendeshaji mpya DART

SERIKALI Septemba mwaka huu inatarajia kusaini mkataba na mwendeshaji mpya wa Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka jijini Dar es Salaam (DART) kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE).

Haya yamebainishwa jijini hapa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa baada ya kuchambua taarifa ya utendaji kazi wa Wakala wa DART.

Silaa alisema hivi sasa mradi huo umekuwa ukiendeshwa kwa kipindi cha mpito na kampuni ya Usafirishaji jijini Dar es Salaam (UDART).

“Wametuahidi kuwa mwanzoni mwa Septemba watasaini mkataba wa makubaliano na kampuni kubwa kutoka nchi za UAE. Kikubwa kamati imeendelea kuwapongeza utakumbuka UDART ilipoanza ilikuwa na tiketi za kielektroniki baadaye ikaingia katika tiketi za mkono,” alisema.

Alisema kwa maelekezo ya Serikali wameanza mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa tiketi ambao unamilikiwa sasa na Serikali, hali ambayo imefanya mapato yaongezeke kutoka Sh bilioni 25 mwaka wa 2020/2021 hadi kufikia Sh bilioni 36 kwa mwaka 2021/2022.

Silaa alisema kamati imeelekeza DART kuendelea kusimamia mapato ya kielektroniki, kuboresha utendaji na kukamilisha mchakato wa kumpata mwendeshaji mpya.

“Tumeiagiza UDART ambayo ni kampuni ya ubia wa wazawa na Serikali kumtengenezea mshindani, ukimtengenezea mshindani wananchi watanufaika ubora wa huduma kwa upande wa nauli na hata huduma wanazozipata zitakuwa zinaenda vizuri zaidi.”

Alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendesha vizuri awamu ya kwanza ya mradi huo ambayo ni kuanzia Kimara kwenda Posta wakati awamu ya pili ya Mbagala hadi Kariakoo ikiwa katika ujenzi.

Silaa alisema awamu ya tatu ya kutoka Kariakoo hadi Gongo la Mboto mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu amepatikana tangu Machi mwaka huu.

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button