Serikali kupeleka polisi kata zote

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema serikali inatekeleza mkakati wa kusogeza huduma za kipolisi kwa wananchi ukiwamo wa kupeleka polisi kwenye kata zote.

Waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Galapo  wilayani Babati mkoani Manyara baada ya kuzindua kituo cha Polisi Kata kilichojengwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali.

Masauni alisema serikali katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 imedhamiria kusogeza huduma za kipolisi karibu na wananchi kwa kujenga vituo vya polisi kata nchi nzima na kupeleka vyombo vya usafiri yakiwemo magari na pikipiki.

“Huu ni mkakati kabambe na pia ni mkakati mahususi na katika kutimiza lengo hilo kuna hatua kadhaa tumeanza kuzipitia, hatua ya kwanza ni kuhakikisha tunapeleka polisi katika kata zote za nchi hii,” alisema.

Masauni alisema mwaka juzi walipeleka mafunzoni askari polisi na kuwapandisha vyeo kwa ngazi ya nyota moja hivyo hatua ya pili ni kutafuta vyombo vya usafiri kwa ajili yao.

“Nataka kuwahakikishia katika Bajeti (2023/2024) tumetenga bajeti ya Sh bilioni 15 na tayari zimeshatolewa na zimelenga kununua magari katika wilaya zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wakuu wa vituo katika wilaya zote waondokane na adha ya kutumia magari mabovu,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu alisema kuna ongezeko la uhalifu, wawekezaji wa vituo vya mafuta, taasisi za fedha zikiwemo benki, kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo na biashara na kuimarisha usalama katika eneo hilo kuwa iliongeza chachu ya ujengwaji wa kituo hicho.

Kamanda Mwakatundu alisema ujenzi wa kituo cha polisi Galapo ulianza mwaka 2007 kwa mawazo ya wananchi wao wenyewe na jengo hilo limejengwa kwa nguvu ya wananchi, serikali na wadau. Alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi 52,982,262.50.

Habari Zifananazo

Back to top button