KAMATI ya Ufundi ya Serikali Mtandao imeanika mikakati mbalimbali inayoonesha namna itakavyotekeleza majukumu yake ya kila siku katika kutumikia umma kwa ufanisi na weledi.
Aidha, mikakati hiyo ni pamoja na kupunguza urudufu wa mifumo pamoja na kuhakikisha kuwa mifumo yote ya Tehama katika taasisi za umma inawasiliana na kubadilishana taarifa kupitia mfumo mkuu wa ubadilishanaji taarifa serikalini.
Mikakati hiyo iliwekwa wazi jana katika kikao cha kwanza cha Kamati ya Ufundi ya Serikali Mtandao kilichofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma na kuongozwa na Kaimu Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tehama, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Eric Kitali.
Kikao hicho ni cha kwanza cha kamati hiyo na kilijadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya utekelezaji wa majukumu yake, ili kuhakikisha jitihada za serikali mtandao zinaimarika na kuleta tija kwa umma.
Makamu Mwenyekiti wa kikao hicho, Kitali alisema kamati hiyo ipo kwa mujibu wa sheria na miongoni mwa majukumu yake ni kutoa ushauri wa kitaalamu, ili kuhakikisha utekelezaji wa Serikali Mtandao unakuwa na tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.
Alisema kamati hiyo ina wajumbe wachache ikilinganishwa na idadi ya wizara na taasisi za serikali zilizopo, na kuwasihi wajumbe wote kutenda haki kwa kuwajibika na kuhakikisha wanatoa ushauri wenye tija katika eneo la Tehama ili kuhakikisha serikali mtandao inaimarika na kuleta tija.
Katibu wa Kamati hiyo, Sylvani Shayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa Tehama katika Serikali Mtandao alisema baadhi ya majukumu ya kamati hiyo ni kupitia na kutoa mapendekezo juu ya Sera ya Serikali Mtandao itakayotekelezwa katika taasisi za umma.