Serikali kushughulika na changamoto za wadau wa habari

SERIKALI itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wa habari katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili zikiwemo sheria zisizo rafiki zinatatuliwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema serikali itafanya kazi na waandishi kwa sababu inatambua mchango wa UTPC katika kunyanyua uwezo wa waandishi wa habari hapa nchini, kuwezesha ofisi za waandishi wa habari mikoani kufanya kazi, kuchochea maendeleo mikoani na kupasha habari wananchi waweze kupata uelewa ili kufanya uamuzi sahihi

Advertisement

“Niko tayari kufanya kazi na UTPC wakati wa shida na raha ninachowaomba msiniangushe mniunge mkono na mimi nitawaunga mkono waswahili wanasema imani huzaa imani, mimi nina imani kubwa na UTPC na ninapenda sana umoja huu kwa sababu ninatambua hapa nilipo ndipo mahali sahihi kwa kuwagusa waandishi wa habari wote bila kujali maeneo walipo,” amesema.

“Moja ya changamoto ni kuhusu sheria zinazohusu vyombo vya habari kwamba inahitaji kurekebishwa, niwahakikishie dhamira ya serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kufanya kazi katika mazingira yote.

“Kwa sasa wizara ya habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia tuendelee na utekelezaji wake,” amesema.

Pia alishauri UTPC kutengeneza mazingira ya kuvutia wawekezaji katika habari kwani hivi sasa vyombo vya habari vingi havilipi mishahara, pia vingi hakuna mikataba ya waandishi wa habari.

“Tunatakiwa tujenge mazingira ambayo watakuja wawekezaji ambao wataona hapo ni mahali pa kuwekeza ili wakiwekeza walipe mishahara,” amesema.

Pia amesema Klabu za waandishi wa habari zinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taaluma ya uandishi wa habari pamoja na kuchangia maendeleo ya mikoa mbalimbali nchini.

“Natoa wito kwa mamlaka mbalimbali za serikali kutosita kuchangia vilabu vya waandishi wa habari wa mikoa isiwe ni kuwakumbuka wakati wa matukio pekee bali kwa wakati wote ikiwemo kipindi ambacho mnatenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza shughuli ambazo mnatambua kuwa zitawashirikisha waandishi wa habari,” amesema.

Awali Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo amesema nchini Tanzania kuna klabu 28, kati ya hizo 26 zipo bara na mbili zipo Zanzibar lengo likiwa ni kuhakikisha waandishi wanakuwa na mazingira wezeshi na salama katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema mkutano huo utakuwa chachu ya kuongeza ufanisi, kuwasemea wasio na sauti, kukosoa pale panapotakiwa na kusifia pale panapotakiwa kusifiwa.

Amesema lengo lililopo sasa ni kuimarisha Klabu za waandishi wa habari Dodoma na Dar es Salaam, ikiwezekana makao makuu ya UTPC yahamishiwe makao makuu ya nchi ili kuwa karibu na viongozi wa serikali na rahisi kufikika na wadau wa habari.